2016-10-29 16:30:00

Kanisa kuu la Mt. Yosefu Mfanyakazi, kutabarukiwa tarehe 5 Nov. 2016


Pale ambapo uhuru wa dini hauzuiliwi Wakristo hujenga majengo kwa lengo la kumwabudu Mungu. Makanisa haya yanayoonekana si mahali tu pa kukutania, bali humaanisha na kuonesha Kanisa lililo hai mahali hapo, makao ya Mungu pamoja na watu waliopatanishwa na kuungana katika Kristo! Kanisa ni nyumba ya sala, ambako Fumbo la Ekaristi takatifu huadhimishwa na kuhifadhiwa; ni mahali pa kukutania waamini na uwepo wa Mwana wa Mungu aliyejitoa sadaka Altareni huheshimiwa, changamoto na mwaliko kwa waamini kujitoa sadaka katika ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mguso wa Kikristo!

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kuwa mwakilishi wake maalum katika maadhimisho ya kutabaruku Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Jimbo Katoliki Karonga, moja ya majimbo tisa yanayounda Kanisa Katoliki nchini Malawi. Ibada ya kutabaruku Kanisa hili itafanyika hapo tarehe 5 Novemba 2016 kwa Ibada itakayoongozwa na Kardinali Filoni kwa kushirikiana na Askofu Martin Anwel Mtumbuka wa Jimbo Katoliki Karonga.

Itakumbukwa kwamba, Jimbo hili lilianzishwa kunako tarehe 21 Julai 2010 na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Kanisa la Bikira Maria likateuliwa kuwa ni Kanisa kuu la Jimbo Katoliki Karonga. Lakini kutokana na athari ya matetemeko ya ardhi yaliyotokea kunako mwaka 2009 na mwaka 2010, Jimbo kwa ufadhili wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu pamoja na juhudi za waamini, likaanzisha mchakato wa ujenzi wa Kanisa jipya mwezi Novemba 2012. Taarifa zinaonesha kwamba, kutokana na umoja na mshikamano wa kidugu, Jimbo Katoliki Njombe, Tanzania lilishiriki kuchangia ujenzi wa Kanisa hili ambalo linatabarukiwa hapo tarehe 5 Novemba 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.