2016-10-28 16:20:00

Wakiwezeshwa, wanawake ni wadau wakuu wa amani na usalama!


Kwa muda mrefu Kanisa limekuwa likitetea umuhimu wa kutoa nafasi ya kutosha kwa wanawake kushiriki katika kutengeneza na kudumisha amani duniani. Wanawake wanaweza kushiriki kikamilifu katika kuzuia vita, mazungumzo ya Kidiplomasia, upatanisho, kurekebisha na kujenga jamii zilizoharibiwa kwa vita na kuepuka kurudi katika machafuko.

Akizungumza katika Umoja wa Mataifa, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican, Askofu Mkuu Bernardito Auza, katika mkutano wa Usalama wa Umoja wa Mataifa, amesisitiza kutambua na kutumia hulka, tabia na uwezo wa wanawake katika kujenga na kudumisha Amani duniani. Katika kufanikisha hilo, ni muhimu wanawake na wasichana kupata nafasi za kutosha katika elimu ya kiwango kinachofaa kadiri ya uwezo.

Elimu, hasa kwa wanawake ina mchango mkubwa ili kuleta Amani katika familia, jumuiya Mahalia na dunia kwa ujumla. Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele katika mashule na vyuo vyake, kuhakikisha elimu bora inatolewa kwa wasichana ambao baadaye wamekuwa watumishi wazuri katika jamii. Hivyo ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuweka msisitizo katika kuelimisha wasichana na wanawake kwa ujumla.

Nia njema ya kutumia karama za wanawake katika kujenga na kudumisha Amani, kunaenda sambamba na juhudi za kuondoa umaskini kati yao, na kuhakikisha wanapata huduma njema za afya sehemu mbalimbali duniani, pamoja na kuhakikisha nafasi za kazi na mishahara stahiki kwa wanawake vinazingatiwa, anasema Askofu Mkuu Auza.

Wanawake wengi hata hivyo wamekuwa wahanga wa ghasia na uonevu, hivyo Askofu Mkuu Auza, anatoa mwaliko wa kutumia rasilimali za dunia ili kuponesha vidonda hivyo kwa wanawake, na kuhakikisha haki inatendeka. Ni bora zaidi kuwekeza katika kumkomboa mwanamke na kumtedea haki kuliko kuwekeza katika silaha za maangamizi, kasisitiza Askofu Mkuu Auza. Kwa kuwa wahanga wengi wa vita na machafuko ni wanawake, haina maana kuwa hawawezi kushiriki katika kutafuta, kujenga na kudumisha Amani duniani. Wanawake wakishirikishwa vema, wakaheshimiwa na kupewa haki zao, ni vyombo bora zaidi vya Amani duniani.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.