2016-10-28 15:33:00

Sala ya Yesu ni msingi wa maisha ya Kanisa!


Msingi wa maisha ya Wakristo ni Yesu wa sala, kwani kila uchaguzi wake, kila ishara, mpaka kifo chake msalabani, maisha ya Yesu yametawaliwa na sala. Ni mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko, katika Misa ya asubuhi siku ya Ijumaa, kwenye Kikanisa kidogo cha Mt. Martha, mjini Vatican, ambapo ametoa wito wa Wakristo wote kujiaminisha katika sala ya Yesu.

Yesu baada ya kukesha mlimani akisali, anashuka na kuchagua Mitume wake kumi na wawili, watakaokaa Naye kujifunza na baadae kuiendeleza kazi ya kutangaza Injili ya Agano jipya; baada ya kushuka toka kusali, wanamuijia watu wengi na anaponya wagonjwa na kufukuza mapepo. Hakika Yeye ndiye Jiwe la msingi la Kanisa, hata hivyo ni Jiwe la msingi lililopiga magoti mbele ya Mungu Baba, katika sala ya kweli na ya rohoni. Yesu tunayemuomba, ni Jiwe la msingi ambaye muda wote yupo mbele ya Baba akituombea sisi wafuasi wake, amefafanua Baba Mtakatifu Francisko.

Yesu anawaombea wafuasi wake, kila mmoja, tena kwa majina. Papa Francisko anaonesha baadhi ya mifano dhahiri ya tabia na maisha ya Yesu katika sala: Yesu alisali hata katika karamu ya mwisho, alisali kabla ya kufanya miujiza, katika mlima wa mizeituni alisali, hata juu ya msalaba alisali. Yesu alimalizia maisha yake hapa duniani akiwa anasali, na leo hii anaendelea kusali, yupo mbele ya Baba Mungu akimuombea kila mmoja kadiri ya mahitaji yake. Yesu wa sala, Ndiye Jiwe la msingi la Kanisa.

Fumbo la Kanisa limejengwa juu ya msingi huo wa sala. Ikumbukwe sehemu ya Injili ambapo Yesu kwa Petro ambaye alimkabidhi Mamlaka ya kulinda Imani ya ndugu zake, ambao ni sisi sote, anamwambia: “Simoni, Simoni, tazama shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano, lakini nimekuombea wewe, ili imani yako isitindike, nawe utakapoongoka uwaaimarishe na wenzako” (Luka 22, 31 – 32). Anachomwambia Petro, Yesu anakwambia pia leo wewe, Yesu anakuambia: ninakuombea kwa Baba Mungu. Ndivyo Baba Mtakatifu Francisko anamkumbusha kila Mkristo kujiaminisha katika sala ya Yesu, aliye Jiwe la msingi la Kanisa, na hivyo kila mmoja ajikite katika sala ya kweli, kila siku na kila wakati.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.