2016-10-28 10:26:00

Huruma ya Mungu inawakumbatia na kuwaambata wote!


Huruma ya Mungu haina mipaka. Huruma yake inawakumbatia wote. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mkamilifu daima na ukamilifu wake huu unaenea hadi katika viumbe vyake. Mwenyezi Mungu anatafuta daima muunganiko ulio mkamilifu na viumbe vyake. Wale walio wema huendelea kuonja upendo wake na wale waliozingirwa na uovu hupata fursa na nguvu ya kurudi tena katika muungano mkalifu na Mungu. Daima tumesikia wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu akituambia “Maana mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana Mungu. Basi ghairini, mkaishi” (Ez 18:32).

Sisi wanadamu ndiyo tunaiwekea mipaka huruma ya Mungu. Kitendo hiki kinaweza kuwa ni sababu ya wale walio wema kuwafungia milango wengine na kuwaona kuwa hawastahili kuipokea huruma hiyo au wale walio katika uovu kukata tamaa na kufunikwa kabisa bila kuiona huruma ya Mungu. Neno la Mungu katika Dominika hii ya 31 ya Mwaka C wa Kanisa linatuonesha urefu na upana wa huruma ya Mungu, sababu na kiu za huruma hiyo na umuhimu wake katika mahusiano yetu na Mwenyezi Mungu.

Mwandishi wa kitabu cha Hekima anatuelezea juu ya kiu hii ya Mungu ya wokovu kwa wote. “Kwa maana wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala hukichukii kitu cho chote ulichokiumba”. Sehemu hii ya Neno la Mungu inaanza kutufunulia kwa kina sababu za Mungu kuhangaikia wokovu wa mwanadamu. Kwanza kabisa ni udhihirisho wa ukamilifu wake na kuthibitisha upendo wake mkuu. Yeye ambaye alimuumba mwanadamu kwa upendo mkuu hatoweza kugeuka na kukichukia kiumbe chake hiki. Ni sawa na kuichukia kazi ya mikono yake au kuweka kasoro katika uumbaji wake. Yeye kila alipoumba alikiona kiumbe chake ni chema sana: “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama ni chema sana” (Mw 1:31). Kwa mantiki ya kawaida kabisa Mungu angehangaikia hiki kiumbe chake kizuri alichokiumba.

Uzuri au wema unatafsiriwa kama ukamilifu. Hii ni ile hali ya kuwa katika uhalisia wake. Mmoja anakisifia chakula kuwa ni kizuri kwa sababu kimekidhi na kinadhihirisha ubora wa ladha yake iliyotarajiwa. Mwanadamu anaudhihirisha uzuri au wema wake pale anapobakia kuwa mwanadamu, yaani anapoutumia vizuri uhuru na utashi wake. Dhambi ilipoingia duniani uzuri na wema huu ulififishwa na matokeo yake ni kuingia katika anguko. Mwanadamu akapoteza ule uzuri wake wa asili na kushindwa kuudhirisha uzuri wake.

Mwenyezi Mungu anasema: “Maana wivu wa nyumba yako umenila, Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata” (Zab 69:9). Wivu huu ndiyo unaonesha sababu ya Mwenyezi Mungu kuuhangaikia wokovu wa mwanadamu kwa kuifunua huruma yake katika Historia nzima ya wokovu wetu na kwa njia ya pekee kupitia mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo aliye Uso wa Huruma ya Mungu.

Mfalme Suleimani anaonesha zaidi sababu ya Mwenyezi Mungu kuifunua huruma yake kuu kwa watu wote: “Ee Mfalme Mkuu, mpenda roho za watu; maana roho yako isiyoharibika imo katika vyote”. Hapa tunakumbushwa uwepo wa Mungu katika viumbe vyake, yaani ulimwengu wote ni mwendelezo wa ukuu na adhama yake. Uwepo wa Mungu umefumbatwa ndani mwetu na pale tunatenda mema tunaufunua upendo wake na kuwa sababu ya kuwaonjesha wengine upendo huo.

Lakini pale tunapozongwa na dhambi tunajikuta mara nyingi tunaufifisha upendo huu. Lakini mwandishi huyu wa Kitabu cha Hekima anatuonesha tendo la upendo wa Mungu la kutupatia fursa ya kuukumbuka tena upendo wake na kuufanya tena hai: “wawaonya, ukiwakumbusha kwa mambo yale yale waliyokosa, ili waokoke katika ubaya wao, na kukuamini Wewe, Bwana”. Hizi ni nafasi mbalimbali za neema ambazo zinatujia, fursa ambazo zinatupatia uwezo wa kimungu unaotusukuma kuuona tena wema wake tulioufifisha kwa dhambi.

Somo la Injili ya Dominika hii linahitimishwa kwa maneno haya: “Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea”. Hitimisho hilo ni uthibitisho kwetu kwamba huruma ya Mungu inawakumbatia wote. Zaidi ya hayo sehemu hii ya Injili inatuwekea mbele yetu changamoto ambazo huwa ni kikwazo kwa kuenea kwa huruma ya Mungu.

Zakayo ambaye anatajwa kama mmoja wa wakubwa wa watoza ushuru anakuwa mbele yetu kama yeye ambaye ana hamu ya kuionja huruma ya Mungu kwa maana “huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani”. Hii ni hatua muhimu katika kuielekea huruma ya Mungu, yaani kuwaka tena ndani mwako ile hamu ya kukutana na Mungu. Bila shaka hamu hii haikutoka hewani tu. Hamu yake hii inaashiria kuwa alikwisha kusikia habari zake: juu ya mafundisho yake, miujiza aliyoitenda na uponyaji alioufanya.

Moyo wa Zakayo ulitamani kumwona Kristo “asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa maana atakuja kupitia njia ile”. Kila neno hapo kutoka kifungu hiki cha Biblia linahitaji ufafanuzi ili kutufikisha katika kuvishinda vikwazo vinaweza kutuzuia au kuwafanya wengine wasiionje huruma ya Mungu.

Umati mkubwa watu unawakilisha jamii inayotuzunguka ambayo inatupatia mambo mengi yasiyotoa nafasi ya kumwona Yesu. Jamii yetu ya kisekulari inatupatia nafasi finyu sana ya kuweza kumwona Yesu. Inatosha sana kuangalia yanayoendelea katika vyombo vya habari na yale yanayopigiwa chapuo kutendeka katika jamii kwa kisingizio cha uhuru na haki ya ubinadamu. Ufupi wa kimo unaendena na hilo la kwanza kwa sababu dunia hii inatupeleka katika uhaba wa kiimani na hivyo kushindwa kumjua Mungu kinagaubaga.

Hatua ya Zakayo kukimbia mbio na kupanda juu ya mkuyu ni hatua kuelekea wokovu. Hapa ndipo inapoonekana nafasi ya neema ya Mungu inayotenda kazi ndani mwetu. Mwanadamu anairuhusu neema ya Mungu impatie nguvu na mwangaza wa kutumia vipaji vyake kusudi daima aweze kumwona Yeye katika yote. Zakayo anatumia vipawa vyake na anatambua kwa ufupi wake anapaswa kupanda juu ndipo atafanikiwa.

Juhudi yake hii inazaa matunda. Anafanikiwa kumwona Kristo na furaha yake haishii hapo tu bali anapokea ugeni wa huyu aliyetamani kumwona: “Zakayo shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako”. Hatua ya Kristo kuingia ndani ya nyumba ya Zakayo kunamwingiza hadi ndani ya moyo wake na kufanya mabadiliko ya maisha: “Tazama Bwana nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimemnyang’anya mtu kitu kwa hila nitamrudishia mara nne”. Ugeni huu unamfunua na kumfanya awe na upendo hata kujawa na ukarimu na kutafuta upatanisho kwa wenzake.

Tendo jema ya wokovu wa Zakayo linaambatana pia na husuda za kibinadamu ambazo mara nyingi huwafumba wengi wasiwafunulie wengine huruma ya Mungu au huingia katika kishawishi cha kuiwekea mipaka huruma ya Mungu. “Hata watu walipoona walinung’unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi”. Kitendo hiki ni kinyume kabisa na wajibu wetu wa kikristo.

Paulo anawafafanulia wakristo wa Thesalonike wajibu huo ambao ni kuomba na kusali kwa wokovu wa watu wote. Mtume Paulo anasema: “Wapenzi, twawaombea ninyi siku zote, ili Mungu wetu awahesabu kuwa mmestahili kuitwa kwenu, akatimiza kila haja ya wema na kila kazi ya imani kwa nguvu”. Huo ndiyo wajibu wetu wa kikristo, yaani kuwa watu wa kuhangaika kwa ajili ya wokovu wetu wote. Tuombe neema ya Mungu katika Dominika hii kusudi tuweze kuwa na utayari wa kuipokea huruma ya Mungu inayotujia bure na pia kuwatangazia wengine huruma hiyo kwani tutambue kuwa sote tu wana wa Ibrahimu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.