2016-10-27 15:44:00

Simameni kidete kupambana na biashara haramu ya binadamu!


Kikundi cha Mtakatifu Martha ni taasisi ya kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu kilichozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2014. Kuanzia tarehe 26 - 27 Oktoba, 2016, kikundi hiki kimekuwa na mkutano wake mjini Vatican, uliokuwa unasimamiwa na Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles. Wajumbe hawa walipata nafasi ya kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 27 Oktoba 2016.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake anasema, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni kati ya changamoto kubwa kwa watu wa nyakati hizi. Kikundi cha Mtakatifu Martha kinachowaunganisha viongozi wa Kanisa na kiraia kinaendelea kutoa mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, wengi wao wakiwa ni watoto wadogo, ambao wanadhalilishwa utu na heshima yao kutokana na umaskini pamoja na kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anasema, hapa ni kazi tu inayotakiwa ili kuweza kupambana na hatimaye, kuondoa mambo yote yanayosababisha biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo sanjari na kuwasaidia waathirika ili kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha yao! Idadi ya waathirika wa biashara haramu ya binadamu inaendelea kuongezeka kila kukicha. Hawa ni watu wanapokonywa utu wao; ukamilifu wa kimwili na kisaikolojia kiasi hata cha kupoteza maisha!

Baba Mtakatifu anawapongeza wajumbe wa Kikundi cha Mtakatifu Martha na kuwataka kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Mwenyezi Mungu atajalia na kuwakirimia neema na baraka kwa wema na ukarimu wanaowatendea wadogo hawa wanaonyanyaswa na kunyonywa; wanaogeuzwa na kutumbukizwa katika utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu anasema, anaendelea kuwasindikiza kwa sala na sadaka yake, ili hatimaye, waweze kufanikisha mapambano haya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.