2016-10-26 10:57:00

Ubalozi wa Vatican ni kielelezo cha umoja wa Kanisa na huduma kwa watu


Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican, hivi karibuni amezindua makazi mapya ya Ubalozi wa Vatican nchini Panamà kwa kusema kwamba, utume wa kidiplomasia unaotekelezwa na Vatican unajikita katika huduma kwa ajili ya Makanisa mahalia kwa njia ya ushirikiano na nchi husika, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Hii ni huduma inayopania pamoja na mambo mengine kuonesha uwepo endelevu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wa Makanisa mahalia na kwa ajili ya watu wote kama kielelezo cha Fumbo la Umoja wa Kanisa unaojidhihirisha kwa njia ya miundo mbinu ya Kanisa pamoja na umoja usionekana uliopo kati ya Mwenyezi Mungu na Kanisa. Ni umoja unaowaunganisha Maaskofu wote chini ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo cha imani, umoja na mapendo ya Kanisa.

Askofu mkuu Becciu amekumbusha kwamba, Vatican ina uhusiano wa Kidiplomasia na Nchi pamoja na Mashirika ya Kimataifa  yapatayo 182, kielelezo cha umoja kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia. Panamà kwa namna ya pekee, inajielekeza zaidi na zaidi katika uhai wa maisha na utume wa Kanisa sanjari na kujikita katika ujenzi wa Jumuiya ya waamini. Kanisa linaendelea kutekeleza dhamana ya Uinjilishaji wa kina kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko pamoja na huduma makini, hususan miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Vatican kwa upande wake, inaendelea kufuatilia maisha na utume wa Makanisa mahalia kwa furaha na matumaini makubwa, ili kusaidia kwa hali na mali mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Andrès Carrascosa Coso, amewashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka hadi kukamilisha ujenzi wa makao mapya ya Ubalozi wa Vatican nchini Panamà. Nyumba hii itasaidia kuendeleza mchakato wa haki na amani jamii. Makazi ya zamani, yatapigwa mnada na fedha itakayopatikana itatumika pia kugharimia maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.