2016-10-24 14:30:00

Changamoto ya Papa Francisko kwa Wayesuit!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 24 Oktoba 2016 ameshiriki katika maadhimisho ya mkutano wa 36 wa Shirika la Wayesuit unaoendelea hapa mjini Roma kwa kuwataka kutembea kwa pamoja katika jina la Bwana, kama watu huru na watiifu wakiwa wameungana katika upendo wa Kristo kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Hii ni hija inayopaswa kutekelezwa kwa moyo mnyofu katika wito, kwa kuwa waaminifu kwa karama ya Shirika, ili hatimaye, kuweza kufika hata katika maeneo ya kiroho na kimwili, ambayo wakati mwingine yanaonekana kuwa na changamoto kubwa.

Baba Mtakatifu Franciko katika hotuba yake amekazia kwa namna ya pekee mambo makuu matatu: Wayesuit waendelee daima kuomba neema ili waweze kuwa ni vyombo vya faraja na furaha katika medani mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote bila kukata wala kukatishwa tamaa na magumu pamoja na changamoto zinazoendelea kujitokeza, daima wakipania mafao ya wengi. Hii ndiyo huduma ya furaha na faraja ya maisha ya kiroho inayojikita katika maisha ya sala.

Mosi, Wayesuit wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Furaha ya Injili kwa kuendelea kukomaa katika fadhila ya matumaini, imani, upendo na furaha ya ndani, mambo ambayo yalikuwa ni chemchemi ya maisha ya Wayesuit wa kwanza. Huu ukawa ni mwanzo wa maisha ya sala ya kijumuiya, utume na ushuhuda wa pamoja kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu. Huu ni mchakato wa kutangaza na kushuhudia Imani inaomwilishwa katika haki na huruma, kwa kuwaendea watu walioko pembezoni mwa maisha ya mwanadamu. Myesuit ni chombo cha furaha kinachotumiwa na Mama Kanisa katika Uinjilishaji kwa kuonesha unyenyekevu na usikivu kwa Roho Mtakatifu na uaminifu kwa Mwenyezi Mungu.

Pili, Baba Mtakatifu anawaalika Wayesuit kuguswa na Yesu Msalabani, ili waweze kumwona na kumhudumia miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni muda muafaka wa kutafakari huduma ya huruma inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu na mwendelezo wa majadiliano na Kristo Msalabani aliyeteswa, akafa na kufufuka ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Yesu kwa huruma yake, amewaona, akawachagua na kuwatuma kutangaza na kushuhudia huruma hii kwa watu wa mataifa wanaoteseka kutokana na ukosefu wa haki; maskini pamoja na wote wanaoendelea kuathirika kutokana na vita. Kwa njia hii, Wayesuit wataweza kuondokana na woga usiokuwa na mashiko, tayari kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo hata katika mazingira magumu na hatarishi!

Tatu, Wayesuiti wajitahidi kujiundia moyo safi, kwa kulisikiliza Kanisa kwa makini zaidi ili kujisadaka kimasomaso kwa huduma makini inayojikita katika unyofu wa moyo, kila mtu akitumia vyema karama ambazo wamejaliwa na Roho Mtakatifu, kwa ajili ya mafao ya wengi. Ili kutekeleza dhamana na wajibu wake, Wayesuit hawana budi kulisikiliza Kanisa kwa kuendelea kujikita katika amani na furaha; kwa toba na wongofu wa ndani tayari kuubeba Msalaba wa Kristo kwa moyo wa unyenyekevu kwa kushikamana na kuandamana na Kanisa, tayari kuwa kweli ni majembe ya Kanisa la Kristo! Hapa kinachohitajika ni umoja na huduma kwa Kanisa.

Wayesuit wakumbuke kuwa, wanafanya hija ya maisha ya pamoja kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani anasema Baba Mtakatifu Francisko. Wanainjilisha na kutamadunisha, ili Kristo Yesu aweze kupewa kipaumbele cha kwanza katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Waendelee kuinjilisha katika umaskini, huduma na bila kumezwa na tamaa za kidunia, tayari kufariji, kuhurumia na kuwasaidia watu kufanya mang’amuzi katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.