2016-10-22 16:29:00

Huruma na majadiliano ni msingi wa amani, upendo na mshikamano!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma, Jumamosi, tarehe 22 Oktoba 2016 wakati wa katekesi yake, amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika mchakato wa huruma na majadiliano, kama ilivyojitokeza kwa Yesu alipokutana na kuanza kujadiliana na Mwanamke Msamaria, kwa kumfunulia undani wa maisha yake na huo ukawa ni mwanzo wa kuambata huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, majadililiano yanawawezesha watu kufahamiana pamoja na kugundua mahitaji ya jirani zao. Ni kielelezo cha heshima inayomwajibisha mtu mwingine kujenga mazingira ya kusikiliza mambo msingi yanayobainishwa na mzungumzaji. Majadiliano ni ishara ya upendo unaotambua tofauti zinazoweza kuwepo, lakini unasaidia kuweka nguvu ya pamoja katika mchakato wa kutafuta na kushirikishana mafao ya wengi. Majadiliano yanawezesha watu kutambuana kama zawadi ya Mungu.

Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, watu wengi kwa sasa wanaishi kila mtu kivyake vyake, hata kama wanazungukwa na jirani zao. Watu wanataka kujionesha na kuwataka wengine kuwasikiliza kwa makini. Hakuna majadiliano ya kweli anasema Baba Mtakatifu Francisko, ikiwa kama hakuna utamaduni wa kusikilizana katika ukweli na uwazi kwani matokeo yake ni kila mtu anataka kuonekana kuwa ni mshindi na huo mara nyingi unakuwa ni mwanzo wa patashika nguo kuchanika. Majadiliano ya kweli yanajikita katika nyakati za ukimya, ili kuweza kukaribisha zawadi ya uwepo wa Mungu katika maisha ya ndugu zao.

Majadiliano yanawawezesha waamini kujenga mahusiano mema yanayofumbatwa katika utu na hatimaye, kuvuka vikwazo vya kutoelewana na kudhaniana vibaya. Kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano ndani ya familia, ili kuweza kurekebisha kasoro zinazoweza kujitokeza katika maisha. Jambo la msingi ni kujenga utamaduni wa kusikilizana kwa makini. Mwelekeo huu utasaidia kuboresha mahusiano kati ya Bwana na Bibi; mahusiano ya dhati kati ya wazazi na watoto wao. Utamaduni wa majadiliano unaweza kuwa na mafao makubwa kati ya walimu na wanafunzi wao; kati ya waajiri na wafanyakazi wao, ili buoresha mazingira ya kazi.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukaza kwa kusema, hata Kanisa linaishi utamaduni wa majadiliano na watu wa nyakati tofauti, ili kutambua mahitaji msingi yaliyomo kwenye moyo wa kina binadamu, ili hatimaye, kuweza kujikita katika mchakato wa kutafuta mafao ya wengi. Mfano hai ni majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi, juu ya uwajibikaji na utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote. Hii ni tema tete hasa kwa wakati huu kutokana na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi.

Majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali ni muhimu ili kuweza kutambua ukweli wa ndani wa utume wake kati ya watu wa mataifa, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa amani pamoja na mtandao wa heshima na udugu. Majadilino yote ni kielelezo cha kiu ya upendo wa Mungu unaowasukuma watu kuutafuta, kwa kila mtu kuchangia tone la wema wake, ili kushirikiana katika kazi Mungu.

Majadiliano yanavunjilia mbali kuta za utengano na hali ya kudhaniana vibaya; yanajenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na wala hakuna mwanya wa baadhi ya watu kubaki wakiwa wameelemewa katika upweke na ubinafsi wao. Baba Mtakatifu anahitimisha kwa kusema, Yesu alifahamu fika yale yaliyokuwa yamefichika moyoni mwa wanamke wa Kisamaria ambaye hakuwa anataka kumfunulia Yesu mambo yake, lakini kwa taratibu aliweza kuingia kwenye Fumbo la maisha ya yule mwanamke Msamaria

Mafundisho haya anasema Baba Mtakatifu, yanapaswa kuvaliwa njuga na kila mmoja wao. Kwa njia ya majadiliano ya kweli waamini wanaweza kukuza alama ya huruma ya Mungu, kwa kuwa ni vyombo vyake vya ukarimu na heshima. Mwishoni ametambua uwepo wa makundi ya wageni na mahujaji waliotoka sehemu mbali mbali za dunia ili kukutana nao kama zawadi ya Mungu ambayo inawasaidia kutajirishana katika maisha. Bikira Maria anawafundisha waamini kusikiliza katika ukimya sanjari na kuyatafakari mambo yote nyoyoni mwao, ili kukidhi shida na mahitaji ya jirani zao. Bikira Maria awe ni mfano bora wa kuigwa katika utoaji wa huduma kwa jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.