2016-10-21 08:42:00

Wanawake katika ujenzi wa amani na utamaduni wa kukutana!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Francesco Cacucci wa Jimbo kuu la Bari, Italia kwa ajili ya washiriki wa mkutano mkuu wa pili kimataifa kuhusu wanawake huko Mashariki ya Kati na Mediterrania ulioanza hapo tarehe 19 – 23 Oktoba, 2016, anawataka wanawake kusimama kidete katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na upatanisho.

Mkutano huu unaongozwa na kauli mbiu “Wanawake wajenzi wa amani kwa ajili ya utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana” na umeandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, Jukwaa la Kimataifa la Wanawake Wakatoliki pamoja na Chama cha Wanawake Wakatoliki Italia. Wajumbe wanashiriki mkutano huu sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu Francisko anawatakia heri na baraka washiriki wote wa mkutano huu na kwa namna ya pekee wanawake wanaotoka huko Mashariki ya Kati na kwenye nchi ambazo zinakabiliwa na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; umaskini pamoja na aina mbali mbali za ubaguzi. Ni matumaini yake kwamba, wigo wa ushiriki wa wanawake katika masuala mbali mbali ya kijamii utapanuka na kuimarishwa, ili kukuza na kujenga utamaduni wa watu kukutana, kufahamiana, kujadiliana na kushikamana ili kujenga matumaini ya amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, mambo yanayochangia katika mchakato wa upatanisho na utulivu kati ya watu wa mataifa.

Baba Mtakatifu anawatakia wajumbe wote wa mkutano huu, nguvu na karama ya Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia kufanya tafakari ya kina itakayozaa matunda ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu anawaomba wajumbe wa mkutano huu, kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.