2016-10-21 08:27:00

Ujasiri wa kimissionari, toba na wongofu wa ndani muhimu katika utume!


Padre Miguel Mirò Mirò, Mkuu wa Shirika la Mtakatifu Augostino Recolleti kwa niaba ya wajumbe wa mkutano mkuu wa 55 wa Shirika waliokutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 20 Oktoba 2016 amemhakikishia Baba Mtakatifu kwamba, wanashirika wamejizatiti kwa ari, moyo mkuu na ushupavu wa kimissionari, kufanya mageuzi katika maisha yao. Wanataka kwa kuanzia kwa Kristo Yesu, ili kujenga moyo wa tafakuri, maisha ya kijumuiya na kimissionari mintarafu karama yao ya Shirika.

Katika mchakato huu wa mageuzi ya maisha miongoni mwa watawa wa Shirika hili, jambo la msingi ni kujikita katika toba na wongofu wa ndani unaofumbatwa katika maisha ya mtawa mmoja mmoja, jumuiya hadi kufikia sera, mikakati na mipango ya shughuli za kichungaji. Bila toba na wongofu wa ndani, mipango yote ya Shirika itashindwa kutekelezwa. Hili ni Shirika ambalo lina jina na historia kubwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa zaidi ya miaka mia nne. Shirika limejikita katika shughuli za kichungaji Parokiani, katika sekta ya elimu pamoja na shughuli za kimissionari sehemu mbali mbali za dunia. Padre Miguel Mirò Mirò anakaza kusema, hadi sasa Shirika lake lina jumla ya watawa 1045 wanaoishi na kutekeleza utume wao katika nchi kumi na tisa. Watawa hawa kwa sasa wanataka kupyaisha karama na moyo wa Mtakatifu Augostino, ili kusaidia kukuza na kudumisha umoja na upendo kwa Mungu na jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.