2016-10-21 15:23:00

Jengeni Kanisa kwa kudumisha umoja, amani na mapendo!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 21 Oktoba 2016 amesema kwamba: unyenyekevu, uvumilivu na upole, kwa kuchukuliana katika upendo kwa kujenga na kudumisha mshikamano ni mambo msingi katika ujenzi wa Kanisa la Kristo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuondokana na chachu ya wivu usiokuwa na mashiko, uhasama, chuki na kinzani kwa kudumisha amani katika akili na nyoyo za waamini.

Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, salam ya amani inamwilishwa katika uhalisia wa maisha yao na wala si kubaki katika maneno matupu kwani haya hayavunji mfupa! Roho mbaya inasababisha vita, chuki na kinzani katika maisha ya watu. Wakristo wanaweza kupata umoja kwa kujikita katika unyenyekevu, uvumilivu, upole na kiasi. Hakuna amani pasi na unyenyekevu! Mahali ambapo kiburi kinatawala hapo kuna machafuko anasema Baba Mtakatifu Francisko, kwani kila mtu anataka kutawala ili kuonesha ubabe!

Bila unyenyekevu hakuna amani na wala hakuna amani pasi na umoja. Kumbe haya ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana katika mchakato wa maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, waamini wanaonekana kana kwamba, wamesahau kuzungumza katika hali ya unyenyekevu, upole na kiasi; mambo ambayo yanaweza kuwasaidia waamini kuvumiliana na kudumisha wito wao mtakatifu kwa kutambua kwamba, kila mtu ana karama na mapungufu yake, kumbe, wanapaswa kuvumiliana na kuheshimiana, ili kujenga na kudumisha kifungo cha amani kiini cha umoja unaoundwa na Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujizatiti kikamilifu katika ujenzi wa misingi ya umoja kwa njia ya kifungo cha amani, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Roho Mtakatifu ni mjenzi wa amani inayowaunganisha waamini kuwa na Bwana mmoja, imani, ubatizo mmoja, Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote. Kifungo cha amani kinakua na kukomaa katika unyenyekevu, uvumilivu na upole, kwa kuchukuliana katika upendo. Mwishoni, waamini wajitahidi kumwomba Roho Mtakatifu ili awasaidie kulifahamu na kuliishi kikamilifu Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.