2016-10-21 09:06:00

Huruma ya Mungu inapenya katika fadhila ya unyenyekevu!


Sala ni nafasi ambayo Mungu anajifunua uso wake uliojaa na huruma na  wakati mwanadamu akipata fursa ya kuionja huruma ya Mungu. Hii ni kwa sababu sala inamkutanisha mwanadamu na Mungu, akiwa peke yake katika altare ya ndani ya moyo wake, mkutano ambao unampatia fursa ya kuzungumza naye kama Baba mwenye huruma kwa kumwomba fadhili mbalimbali, kumwomba msamaha na kutumtukuza na pia kushukuru kwa fadhila zake anazotumiminia kila uchao. Sala ni fursa yetu sisi wanadamu katika hali yoyote, iwe ni wakati wa furaha au wa huzuni, wakati wa mafanikio au matatizo, ya kuufanya hai uwepo wa Mungu kwetu na kumpatia nafasi inayostahili kama Bwana, Mfalme na Mkuu wa maisha yetu.

Maandiko matakatifu ya Dominika hii yatuwekea mbele yetu muktadha wa watu wawili wanaokwenda hekaluni kusali. Watu hawa wanatupatia fundisho kubwa juu ya maana halisi ya sala. Mbele yetu tunawekewa Farisayo anayejisikia mkamilifu mbele ya Mungu na kuidai huruma ya Mungu na kwa upande mwingine Mtoza ushuru anayejiweka mbele ya Mungu katika hali ya unyenyekevu kuijongea huruma ya Mungu. Mafundisho makubwa mawili yanajitokeza katika Dominika hii, hususani huruma ya Mungu. Kwanza kabisa tunaoneshwa kwamba huruma ya Mungu ni zawadi ambayo hatuna sababu ya kuidai kama haki yetu. Majigambo ya huyu Farisayo ni kujihesabia haki mbele ya Mungu. Ni sawa na kusema mbele ya Mungu kwamba nimetimiza amri zako na sasa nipatie iliyo haki yangu. Hili ni onyo kwetu katika maisha yetu ya imani ambayo yanachuchumilia kupata tuzo tu.

Fundisho la pili tunalolipata katika Dominika hii ni ile hali ya kujiona bora kuliko wengine. “Mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru”. Huruma ya Mungu ina hulka ya kuwatazama na kumbatia wote. Hii ni kwa sababu jicho la Mungu lenye huruma linamtazama mwanadamu kiumbe kikamilifu ambacho ni kazi ya mikono yake, kiumbe ambacho sasa kimechafuliwa na uovu wa kidunia. Hii ndiyo maana daima Mungu anawaka wivu dhidi ya mwanadamu anayeingia katika uovu. Anajua kwa hakika shetani hawezi kuiharibu wala kuigusa hadhi yake ya asili na hicho ndicho anachokitazama, yaani anamtazama mwanadamu, mbele yake anamwona mwanadamu na sio mzinzi, mnyang’anyi au mdhalimu. Maneno haya “mimi si kama watu wengine...” ni hali ya kutaka kuiwekea mipaka huruma ya Mungu. Ni kusudio la kumtaka Mungu kuwaangalia wale wanaotenda kadiri ya Neno lake tu na kamwe asiwaangalie wadhambi. Hatua hiyo ni kusudio ya kuhukumu wengine na kujikinai haki kwa mwanadamu.

Katika somo la pili Mtume Paulo anaonesha uaminifu wake katika kulishika neno la Mungu bila kujitenga na wanadamu wenzake au kuwahesabia ubaya. “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza imani nimeilinda ... katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha ... nami nikaokolewa katika kinywa cha simba”. Mtume Paulo anatufundisha nini hapa? Kwanza ni utegemezi kamilifu kwa Mungu. Mwanadamu anapaswa kuwa katika muunganiko wa daima na Mungu katika hali zote. Pili mtume Paulo anatufundisha kuepa daima kuwaangalia wengine wanakutendea nini.

Hali hii ya kuanza kuwatazama wengine mara nyingi hutufikisha katika kujilinganisha nao na kwenda mbali zaidi kwa kujiona ubora kuliko wengine. Mtume Paulo angeweza kuwadharau au kuwachukia watu hao kwa kujidai kwamba yeye katika utume wake alistahili kufarijiwa lakini anasema “naomba wasihesabiwe hatia katika hilo”. Hawaoni kuwa ni wasaliti ambao wamemwacha bali anawaombea Huruma ya Mungu. Hapa tunaliona dai lingine la huruma ya Mungu, yaani kuwa na utayari wa kushirikishana tone hilo la huruma ya Mungu. Paulo anatufundisha kwa vitendo kinyume na Farisayo yule ambaye anamwangalia mwenzake kama mdhambi.

Huruma ya Mungu si haki yetu bali ni tendo la upendo wa Mungu kwetu. Tunapokaribia kuhitimisha mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu ni vema kuliweka vema wazo hilo vichwani mwetu. Hii ni kwa sababu ipo hatari inayotunyemelea na wakati mwingine kutufanya kukurupusha wajibu wetu wa kuijongea huruma hii katika hali inayostahili, yaani kwa imani na unyenyekevu. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma. Neno moja analitaka kutoka kwa mimi na wewe: kumtambua Yeye katika ukuu wake kama ulivyo na kuijongea huruma yake kwa unyenyekevu. Hekima ya Yoshua bin Sira inatufafanulia jinsi ambavyo Mungu anawaangalia wanyonge na wanyenyekevu bila kujali cheo cha mtu. Bin Sira anatuambia kwamba Mungu yu karibu ya walio fukara na wanyonge.

Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inatupeleka katika moja ya Heri nane zinazotajwa na Krsito katika Injili kwamba: “... walio maskini wa roho, ... ufalme wa mbinguni ni wao”. Ni umaskini huu ambao unafafanua nini maana ya unyenyekevu. Maskini rohoni daima anasikia ulazima na umuhimu wa Mungu na bila Yeye hujiona hawezi kitu. Hili ndilo linalokosekana kwa Farisayo. Bin Sira anahitimisha kwa kutuambia kwamba: “Sala yake mnyenyekevu hupenya mawingu; wala haitatulia hata itakapowasili; wala haitaondoka hata Aliye juu atakapoiangalia, akaamua kwa adili, akatekeleza hukumu”. Huruma ya Mungu inapenya  na kustawi katika unyenyekevu.

Mara nyingi hali ya kujidai ukamilifu utupeleka katika kupoteza sifa ya kuwa udongo mzuri wa kuistawisha huruma ya Mungu. Kudai haki kunafunga masikio, macho na mioyo yetu na hivyo kukosa upendo kwa wengine. Zaidi ya hayo kunatujengea kiburi na kutaka kuonekana mbele ya jamii ya watu kuwa tu watu wema. Farisayo tunayepewa mfano katika somo la Injili anatudhihirishia hili: “mimi si kama watu wengine”. Kifungu hiki cha maneno kinamtenga na wanadamu wenzake na kudai mbele ya Mungu aonekane hivyo. Mara ngapi tunaingia vishawishi vya kutafuta umaarufu ndani ya jamii au hata ndani ya jumuiya ya kikristo kwa kujifananisha na wengine? Inatosha sana kufuatilia linaloendelea kipindi hiki katika Taifa la Marekani. Taifa hili lenye nguvu kubwa ya kiuchumi lipo katika mchakato wa kumpata kiongozi wao mwingine lakini katika kampeni za wagombea wa nafasi hiyo kumejaa vijembe na kukashifiana tu. Kamwe haionekani lugha ya kibinadamu ya kumzungumzia vema mpinzani wako. Ni kujiona kuwa nina haki zaidi ya mwingine: “mimi si kama watu wengine”.

Huruma ya Mungu inatualika kujivika unyenyekevu. Ni wajibu wetu kujongea mbele ya Mungu tukiwa katika hali ya kujishusha na kujivika upendo. Tutambue kwamba huruma ya Mungu ni kwa wanadamu wote na inawatafuta wote. Tuepe kuwa mahakimu wa watu wengine ili sisi kuonekana wema zaidi. Kwa Mungu ni furaha wote kupata wokovu. Yeye yupo tayari kuwaacha kondoo tisini na kenda nyikani kwa ajili ya kumpata mmoja aliyepotea hivyo tuepuke kishawishi cha kumchagulia wale wanaostahili huruma yake. Daima twende mbele yake tukisema mithili ya mtoza ushuru: “Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi”.

Kutoka Studio za Redio Vatikani ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.