2016-10-21 16:19:00

Achana na Mafarisayo uchwara wanaojishebudua!


Leo ni patashika nguo kuchanika! Farisayo uchwara anakutana na mtoza ushuru, kila mtu anangalia mwenzake kwa jino pembe! Lakini zaidi fuatilia kisa hiki, kwani ukitaka kujua utamu wa ngoma, jichanganye mwenyewe! Chachu au hamira ni kitu kama dawa inayochochachisha. Kwa wapika pombe za ulezi au mhogo chachu hiyo inaitwa “ngandu.” Ndiyo maana kuna msemo: “Bila chachu ya ulezi pombe buzaa haiwi.” Kwa kawaida Chachu huwa kidogo lakini inaumua pombe au donge la ngano. Katika maadili, chachu ni mchocheo wa kutenda uovu. Yesu anatumia msamiati wa chachu kuwataadharisha Wanafunzi wake dhidi ya matendo mabovu ya Mafarisayo: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na ya Herode” (Mt. 8:14, au “Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo” (Mt. 16:6) yaani wajiepusha na unafiki na mafundisho yao (Mt 12:1; 16:12).

Leo, Yesu anatuonesha “Live” hiyo chachu inavyofanya kazi kwa kutupatia mfano wa Farisayo na Mtozaushuru. Hatari iliyoko kwetu katika mfano huu ni kwamba tunaweza kujilinganisha na mtu asiyetakiwa tujilinganishe naye. Mathalani, mtu huwezi ukajilinganisha na Farisayo anayetajwa hapa kwa vile anaonekana kuwa ana majivuno, anajiona na kujikweza. Kumbe ni rahisi kujilinganisha na Mtoza ushuru ambaye hata kama alikuwa mwovu na mbaya, lakini ni mnyenyekevu, mnyofu na amejuta uovu wake. Kwa hiyo leo Mkristu unaweza kujisikia vizuri kwani umeshika kikamilifu ujumbe wa Kristu kama  huyu mtoza ushuru unapojipiga kifua na kusali “Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana.”

Kabla ya kuwaona wahusiaka wa mfano huu, tuangalie kwanza mazingira yalivyokuwa. Injili inaanza hivi:“Yesu aliwaambia mfano huu watu waliojikinai kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote.” Hapa yaonekana mfano unatugusa sisi sote. Halafu tunaambiwa kuwa: “Watu wawili wapanda kwenda hekaluni kusali. Hekaluni ni pahala pa kuonana na Mungu kama asemavyo Mzaburi, pindi Waisraeli wako utumwani wakisali: “Lini nitarudi (Yerusalemu) kuuona uso wa Mungu.” Hadhi yao:“Mmoja Farisayo, wa pili Mtoza ushuru.” Wanawakilisha matabaka ya watu waliokuwepo katika Taifa la Wayahudi. Kisha tunaambiwa jinsi kila mmoja wao anavyomwona Mungu kama wasemavyo wapembuzi: “Niambie unavyosali nami nitakuambia wewe ni mtu wa aina gani, yaani unayo mahusiano ya aina gani na Mungu.”

Tahadhari! Fikira potovu tulizojengewa juu ya mfarisayo kwamba ni mnafiki na mwongo. Kumbe kwa Waisraeli, Mfarisayo alikuwa mtu wa haki, mfuata dini, anafuata kidhati imani yake, anafuata masharti ya dini na ya Tora, kama mtume Paulo alivyojivunia kuwa ni Farisayo halisi anayefuata dini, akaongea vizuri juu ya mafarisayo kwamba walimfuata Bwana kwa dhati. Hata Yesu mwenyewe hakumgombeza Farisayo Nikodemu alipoonana naye.

Kadhalika hata ukimfuatiliA Farisayo yule kwa karibu alipoingia Hekaluni hutakuta kasoro: “Yule Farisayo akasimama.” Kwa Myahudi ilikuwa kawaida kusimama wakati wa sala kwani hata mtoza ushuru alisimama. Kisha Farisayo akaanza kusali: “Akaomba hivi moyoni mwake.” Kwa kigiriki ni “pros heauton, maana yake ni “kujielekea mwenyewe.” Halafu tauta proseucheto ni kusali yaani “Alijisalia mwenyewe.” Yaani, Farisayo alisimama mbele ya uso wa Mungu hekaluni lakini ilkuwa kama mtu anayejiangalia katika kioo na kujipembua akisema: “Mungu ninakushukuru.” Kushukuru ni sala nzuri sana tunaposimama mbele ya Mungu. Farisayo huyu anamshukuru Mungu kutokana na mastahili mengi aliyoyapata.

Kwamba Mungu amemweka katika njia iliyo sawa. Ukiiangalia kwa makini sala hii, utamwona Farisayo huyu kuwa ni mtu wa haki, mnyofu, anayefuata Tora, aidha ni mtu wa maadili. Labda kasoro ndogo inajitokeza pale anapojilinganisha na wengine anaposali: “kwani mimi siyo kama watu wengine. Wevi, hawana haki, na washarati.” Kama sala hii ningemtungia mimi ingeweza kusema hivi: “Ee Mungu, ninakushukuru sana. Aidha ninafuraha sana kwa sababu kwa kukusikiliza wewe na kuupata mwanga wa Neno lako, ninaweza kuishi kwa furaha, kwani yote umenifadhilia. Kwa bahati mbaya huyo mwenzangu aliyesimama nyuma ya kanisa amekosea njia, ndiyo maana hana furaha, anajipigapiga tu kifuani, watu wote wanamkwepa. Kama ungeniangazia namna ninavyoweza kumsaidia angalau kumpa neno zuri ningalifanya. Kwa vyovyote mimi binafsi ninakushukuru kawa sababu niko katika njia sawa.” Farisayo huyu anasali akitambua kuwa amepewa fadhili za Mungu zinazomwezesha kuishi maisha mazuri na ya furaha.

Aidha anaendelea kujipembua akiorodhesha matendo ya sadaka anayofanya: Mosi,“Mimi ninafunga mara mbili kwa juma;” Kwa kawaida mfungo ulikuwa siku ya Yom Kippur walipotakiwa kufunga hata maji kwa masaa ishirini na matano. Aidha kwa mwaka kulikuwa nyakati nne za kufunga. Lakini Farisayo huyu alifunga mara mbili kwa wiki, Jumatatu na Alhamisi. Katika mfungo huo aliwaombea watu wasilaaniwe na Mungu. Pili alitoa pia sadaka: “Natoa zaka katika mapato yangu yote.” Kwa kawaida mapato hayo yalitokana na shukrani ya mazao ya ngano, ya zabibu, na limbuko la kwanza la mifugo. Kuhani pia ilibidi atoe sehemu ya kumi ya mapato yake, lakini Farisayo huyu alitoa sehemu yote ya mapato yake kupita idadi aliyotoa mkulima pamoja na kuhani. Jinsi Farisayo huyu alivyokuwa mtu wa haki asiye na kosa mbele ya Mungu na mbele ya watu, mmoja huwezi kuona kasoro au ubaya wowote ule toka kwake. Kwa hiyo ni kwa haki kabisa kushukuru na kujivunia maisha mazuri aliyopata kwa Mungu.

Kumbe, Mtoza ushuru alikuwa na maisha tofauti. Kadiri ya sheria, kazi ya Mtozaushuru ilikuwa kukusanya kodi za mapato na kuilipa serikali. Lakini sheria ilimruhusu pia kutoza kodi nyingi ili kupata pesa zaidi. Kwa hiyo Watozaushuru ni wevi waliohalalishiwa wizi na serikali. Watu waliwachukia Watozaushuru siyo kwa sababu walikuwa wevi la hasha, bali kwa vile walikuwa wanashirikiana na serikali inayowakandamiza raia wake. Mapato yake watu waliwakwepa, hawakuwaamkia wala kuwakaribisha majumbani mwao. Mahakamani hawakuwaamini kwa vile walijulikana kuwa ni waongo. Talmud inasema kwamba ili kuokoka iliwabidi Watozaushuru warudishe kila kitu walichokichukua na nyongeza ya asilimia ishirini. Juu yao hata Yesu anasema: “Ni rahisi kwa ngamia kupenya tundu la sindano kuliko tajiri kuingia paradisini.”

Tukizingatia suala la maadili, kibinadamu tunaweza kuhitimisha mfano huu kwa namna hii: Mfarisayo ni mfano wa kuufuata, ingawaje ndiyo inatakiwa ajifunze kuwa mnyenyekevu. Lakini kwa vyovyote Farisayo anasubiri paradisi. Lakini, Mtozaushuru siyo mfano mzuri wa maadili, ni dhahiri hana mahusiano mazuri na Mungu na binadamu wenzake hata kama alijuta. Kabla ya kuingia Paradisini inambidi alipe yote aliyoyafanya. Lakini kumbe, Yesu anahitimisha mfano huu tofauti kabisa.

Hapa hatushughulikii suala la maadili mabovu ya Farisayo au mabovu ya Mtoza ushuru, la hasha bali tunaangalia mahusiano waliyokuwa nayo na Mungu. Kwa hiyo, chachu mbovu ya Farisayo ililala katika mahusiano yake na Mungu. Kwa sababu ingetosha kwake amshukuru Mungu basi na kurudi nyumbani. Lakini yeye anaenda hekaluni na kusimama mbele ili kuonesha kuwa anastahili kila kitu. Mapato ya mahusiano namna hiyo na Mungu, huzaa mahusiano mabaya na wengine, yaani unawaona kuwa ni waovu, hawana haki, ni wevi na washaratishaji tu. Mahusiano hayo ndiyo yanayoweza kuwaathiri pia wafuasi wa Kristu. Ingawaje Yesu alibadili aina hiyo ya mahusiano na Mungu lakini roho hiyo imebaki bado ndani ya jumuia ya wafuasi wa Kristo.

Mtoza ushuru, alifahamu mahusiano yatakiwayo na Mungu, alijiona hastahili chochote, hivi anasimama mbali. Alijitambua alikuwa mbali na Mungu hata na jamii, ndiyo maana anasimama mbali akijitenga mwenyewe na Mungu na Mfarisayo. Anaomba akiinama kichwa na hakuthubutu kuinua macho yake kwa Mungu kuonesha kuwa hakustahili. “Akakigonga kifua chake.” Kifua ni alama ya uchaguzi. Hivi anagonga kifua kuonesha amejitambua mwenyewe kuwa alikosea sana katika kuchagua aina ya maisha. Sala yake inakuwa fupi tu: “Bwana unisamehe mimi mkosefu.” Kwamba wewe Bwana, una namna yoyote ile ya kuniokoa na kunikaribisha kwako, kwani nimetambua kwamba nilikuwa mbali na wewe.

Mtoza ushuru, alisali akijua hali yake, hivi alimpa Mungu uwezekano wa kumgeuza na kumwongoza katika njia ya wokovu. Kumbe mfarisayo, amerudi nyumbani kama zamani akijiona anayo maisha mazuri, safi, ya haki hivi Mungu hana nafasi yoyote ile katika maisha yake. Mapato yake ni kutengeneza mpaka kati ya wenye haki na watenda dhambi. Mbele ya Farisayo yule hata Mungu aligeuzwa kuwa Farisayo anayewatenga wenye haki na wadhambi. Hii ndiyo hatari ya chachu ya wafarisayo. Yesu anahitimisha: Mtoza ushuru alirudi nyumbani amehesabiwa haki. Hebu nasi tujiunge tena na aya ya kwanza ya mfano huu: “Yesu aliwaambia mfano huu watu waliojikinai kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote.” Hapa tunaelekezwa sisi Wafarisayo mamboleo yaani sisi Wakristo. Yesu anayo wasiwasi na ufarisayo huo, kwa vile unafanya mahusiano na Mungu yawe mabovu na hatimaye kudharau wengine na kuwabagua wengine.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.