2016-10-20 15:28:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Maadhimisho ya Siku ya Kimissionari Duniani


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni nafasi muhimu sana kwa waamini kuangalia mchakato wa utangazaji wa Habari Njema kwa watu wa mataifa kama tendo kubwa la huruma ya Mungu kiroho na kimwili. Maadhimisho ya Siku ya 90 ya Kimissionari Duniani, tarehe 23 Oktoba 2016 ni mwaliko kwa waamini wote kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu kwa watu wa mataifa kila mtu akijitahidi kutumia karama na mapaji aliyokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya familia ya Mungu.

Kanisa bado litaendelea kuwahudumia hata wale wasiofahamu bado Habari Njema ya Wokovu, kwani linatamani kwamba, watu wote waweze kuokoka, ili hatimaye, waweze kuonja upendo wa Mungu. Kanisa lina utume wa kutangaza huruma ya Mungu kwa ari na moyo mkuu, ili iweze kupenya katika akili na nyoyo za watu wote. Huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu pale anapokutana na binadamu, tangu kuumbwa kwake, kwani anataka kuonesha ukuu wake kwa wanyonge, wadogo na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha Mama anayewajali, anayewapenda na kuwatunza watoto wake kwani hawa ni wazawa wa tumbo lake.

Hii ndiyo rutuba inayoshibisha watoto wa Mungu hata katika udhaifu na ukosefu wa uaminifu, kwani Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo. Huruma ya Mungu inapata utimilifu wa ufunuo wake kwa Neno aliyefanyika mwili anayedhihirisha Uso wa huruma ya Mungu mintarafu mifano ya huruma ya Mungu kadiri ya Injili. Hivi ndivyo anavyoandika Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 90 ya Kimissionari Duniani kwa Mwaka 2016 inayoongozwa na kauli mbiu “Kanisa la kimissionari, shuhuda wa huruma”.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kupokea huruma ya Mungu kwa kumfuasa Kristo, kusoma na kutafakari Injili; kwa kuadhimisha Sakramenti za Kanisa na kwamba, kwa njia ya msaada wa Roho Mtakatifu waamini wanaweza kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni, kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Waamini wajifunze kupenda kama anavyopenda Baba wa mbinguni kwa kujisadaka ili maisha yao yawe kweli ni kielelezo cha wema wa Mungu, kwa kuanzia na Kanisa lenyewe linaloishi na kumwilisha huruma ya Kristo, anayeliangalia kwa upendo wenye huruma ambao unakuwa ni chemchemi ya utume wake wa kuwashirikisha  watu wengine kwa njia ya majadiliano yanayojikita katika heshima kwa tamaduni na imani za watu wengine.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kushuhudia huruma ya Mungu katika maisha yao kama ilivyokuwa kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo, kielelezo cha huruma ya Mungu kinachoshuhudiwa na watawa wanaotangaza Habari Njema ya Wokovu katika nchi za kimissionari kwa njia ya huduma makini. Wamissionari hawa wanainjilisha na kuwagawia waamini Mafumbo ya Kanisa sanjari na kuhudumia Injili ya uhai kwa kutumia rasilimali mbali mbali za maisha ya kiroho na kimwili zinazopatikana mbele yao, katika mchakato wa ujenzi wa mahusiano mema, utulivu, amani, mshikamano, majadiliano, ushirikiano na udugu katika medani mbali mbali za maisha, daima maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wakipewa kipaumbele cha kwanza.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, huduma ya kimissionari katika sekta ya elimu ni kati ya mambo ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee katika kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu. Majiundo makini yanayojikita katika Uinjilishaji yamewasaidia wengi kuweza kuifahamu Injili. Kwa njia hii, Kanisa linaweza kutambulikana kama Mama hata kwa wale ambao wataweza kuzaliwa hapo baadaye katika imani. Kwa njia ya Injili ya huruma ya Mungu, Kanisa litaweza kuwafikia watu wengi zaidi, ili kuwawezesha kupokea zawadi ya imani kutoka kwa Mungu na wala si  matunda ya wongofu wa kulazimishana. Imani inaweza kukua kutokana na upendo wa ushuhuda wa wainjilishaji wa Kristo; ushuhuda wa upendo ambao hauna mipaka wala ubaguzi unaobubujika kutoka kwa Kristo aliyejisadaka maisha na upendo wake kwa binadamu wote.

Kila mtu anasema Baba Mtakatifu ana haki ya kupokea zawadi ya imani ili kupambana na ukosefu wa haki msingi, vita na kinzani za kibinadamu ambazo kimsingi zinasubiri majibu muafaka kutoka kwa waamini. Wamissionari wanatambua kwamba Injili ya msamaha na huruma ya Mungu inaweza kuwakirimia watu furaha; upatanisho, haki na amani, kwani Kanisa linatumwa kuwatangazia watu wote Habari Njema ya Wokovu. Huu ni mwaliko kwa Wakristo wote kujizatiti katika kukabiliana na changamoto hizi kwa njia ya upyaisho wa shughuli na mikakati ya kimissionari, ili kuwaonjesha watu wanaoishi pembezoni mwa jamii mwanga wa Injili.

Kanisa linaadhimisha Siku ya 90 ya Kimissionari Duniani, iliyoanzishwa na Papa Pio wa Kumi na moja kunako mwaka 1926. Ikumbukwe kwamba, matoleo yote katika Jumapili hii kutoka kwa Wakristo yanapaswa kuchangia huduma kwa Makanisa hitaji sehemu mbali mbali za dunia, ili kutangaza na kushuhudia Injili hadi miisho ya dunia. Hiki ni kielelezo anasema Baba Mtakatifu cha umoja wa Kanisa la Kimissionari, kwa kusaidia huduma kwa binadamu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.