2016-10-20 09:09:00

Majadiliano kuhusu hatima ya wasichana wa Chibok yanaendelea!


Serikali kuu ya Nigeria inaendelea kujadiliana na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram ili kuangalia uwezekano wa kuwaachilia zaidi wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Chibok waliotekwa nyara mwezi Aprili, 2014. Haya yamebainishwa na msemaji wa Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria. Baada ya kikundi cha wasichana 21 kuachiliwa huru, kwa sasa mazungumzo yanaendelea ili kuangalia uwezekano wa kuwaachilia wasichana wengine 80 ambao bado wanashikiliwa na Kikundi cha Boko Haram.

Wengi wa wasichana hawa kutokana na aibu ya kukataliwa na kutengwa na jamii wanaogopa kurejea tena nyumbani kwao. Wachunguzi wa mambo wanasema, baadhi ya wasichana hawa tayari wamekwishasilimishwa na kujengewa mazingira magumu na hatarishi, hali ambayo inakuwa ni vigumu kuweza kurejea tena katika hali ya maisha ya kawaida. Wengi wao wamenyanyaswa kijinsia na kulazimishwa kuolewa na wanajeshi wa Boko Haram, sasa wana watoto.

Baadhi yao wamelazimika kwenda kusoma nje ya nchi ili walau kuweza kupata amani na utulivu wa ndani baada ya mateso makali waliyokumbana nayo tangu walipotekwa nyara kunako mwaka 2014. Baada ya kutekwa nyara wasichana hawa walitengwa katika makundi makuu mawili, kundi moja ni lile ambalo lilikubali kuongokea dini ya Kiislam na wale ambao walikataa waligeuzwa na hatimaye, kutumbukizwa kwenye utumwa mamboleo. Kuna baadhi ya wasichana walionesha msimamo wa kutokubali kutumia na Boko Haram katika kutekeleza vitendo vya mauaji na uvunjifu wa amani nchini Nigeria. Wasichana walioachaliwa Jumatano tarehe 19 Oktoba 2016 wamekutana na kuzungumza na Rais Buhari. Serikali ya Nigeria inafanya mazungumzo na Boko Haram yanayoratibiwa na Chama cha Msalaba Mwekundu, kilichosaidia pia kuachiliwa kwa baadhi ya wasichana hawa hivi karibuni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.