2016-10-19 15:15:00

Vijana wanahamasishwa kuthamini na kupenda wito wa Kipadre


Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri kuanzia tarehe 19 Oktoba 2016 limezindua Kongamano la Kimataifa kuhusu Miito linaloongozwa na kauli mbiu “Akamwangalia kwa huruma, akamchagua” “Miserando atque eligendo”. Hali ya miito ya Kipadre, Mafundisho Tanzu ya Kanisa kuhusu miito, Utume wa Kikasisi na Shughuli za kichungaji kwa ajili ya miito ni kati ya mada zinazojadiliwa kwa kina na mapana, ili kuwahamasisha vijana kuweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani!

Askofu mkuu Jorge Carlos Paròn Wong, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, kongamano hili linahudhuriwa na viongozi 300 wa Kanisa kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kongamano hili ni sehemu pia ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu itakayoadhimishwa mwezi Oktoba 2018 kwa kujikita katika mambo makuu matatu: Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito.

Tema hizi ni muhimu sana katika uhamasishaji na malezi ya miito mbali mbali miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kufikia ukomavu katika maisha yao ya kiutu na kiroho, na hatimaye, kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kwa njia ya wito na maisha ya Kipadre na Kitawa. Mang’amuzi ya wito wa kipadre yanapata chimbuko lake kutokana na upendo wenyenye huruma unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kijana anapoonja huruma na upendo huu, anatambua kwamba, kweli anaitwa kwa njia ya pekee kujisadaka katika maisha ya huduma.

Changamoto kubwa katika uhamasishaji wa miito mitakatatifu miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ni kuwa karibu na kutembea pamoja nao katika uhalisia wa maisha, ili waweze kufanya kweli maamuzi machungu katika maisha; maamuzi ambayo yatawasaidia kuwa na furaha ya kweli, kwa kutambua na kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao na hatimaye kujibu upendo huu kwa ukarimu, uaminifu na mapendo ya dhati.

Askofu mkuu Wong anakaza kusema, licha ya changamoto nyingi zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia lakini bado kuna vijana wengi wa kizazi kipya wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Vijana wengi ni wale ambao wameguswa kwa namna ya pekee na ushuhuda wa maisha unaotolewa na Mapadre na watawa katika medani mbali mbali za maisha kwa njia ya furaha, upendo na matumaini. Katika ulimwengu huu ambao umegeuka kuwa kama tambara bovu, bado Roho Mtakatifu anaendelea kutenda miujiza kwa kuamsha ndani ya vijana wa kizazi kipya hamu ya kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani kwa njia ya huduma kwa Mungu na jirani.

Wajumbe wa mkutano huu, baada ya kupita katika Lango la huruma ya Mungu na kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Ijumaa watakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye anapokutana na Wakeri pamoja na majandokasisi anazungumza nao kutoka katika undani wa sakafu ya moyo wake. Changamoto kubwa inayowagusa vijana wengi ni ushuhuda wa maisha yake yenye mguso na mvuto; huruma na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kumbe, Baba Mtakatifu anawaalika Mapadre na Watawa kuwa kweli ni majembe yenye mvuto na mashiko, tayari kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kuweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao; kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu katika maisha ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.