2016-10-19 11:21:00

Jengeni na kuimarisha sera na uchumi unaomjali binadamu!


Utamaduni wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu ni chimbuko la uchumi unaoendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya binadamu, changamoto ni kuanza mchakato mpya wa sera na uchumi unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi, ili kupambana na baa la umaskini linalonyanyasa utu na heshima ya binadamu. Azma hii inawezekana ikiwa kama watu wanafanikiwa kupata mikopo yenye masharti nafuu, ili kujijengea uwezo wa kiuchumi.

Haya ni mawazo makuu yaliyotolewa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati alipokuwa anashiriki kwenye Kongamano la Tatu kwa Bara la Ulaya kuhusu Mikopo midogo midogo, lililofunguliwa rasmi mjini Roma, Jumatano tarehe 19 Oktoba na linatarajiwa kuhitimishwa Ijumaa, tarehe 21 Oktoba 2016. Kongamano hili linaongozwa na kauli mbiu “Uchumi wa kijamii wa soko, mikopo midogo midogo na mapambano dhidi ya umaskini”.

Hii ni tema ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameipatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kweli sera na mikakati makini ya kiuchumi isaidie mchakato wa kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, badala ya kutafuta faida kubwa ambayo imekuwa ni chanzo kikuu cha athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa sanjari na uchafuzi wa mazingira.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, binadamu na mahitaji yake msingi anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza badala ya kuendelea kutumbukia katika baa la njaa, magonjwa na umaskini wa hali na kipato, mambo ambayo pengine kwa sasa hayana kipaumbele katika vyombo vya habari kimataifa kwani yamezoeleka! Uchu wa fedha na utajiri wa haraka haraka ni mambo hatari kwani yanaendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu pamoja na uchafuzi mkubwa wa mazingira ambao athari zake zinaonekana katika uso wa dunia, lakini wanaoteseka zaidi ni maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi!

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujielekeza katika ujenzi wa uchumi jamii, ambamo binadamu anapewa msukumo wa pekee katika sera na mipango yote ya kiuchumi anasema Kardinali Turkson. Lengo ni kuibua uchumi wenye mwelekeo mpya unaojikita katika utu, mahitaji msingi ya kijamii na kwamba, huu ni uchumi unaopaswa kuwa ni shirikishi ili kupambana na changamoto mamboleo zinazotokana na ukosefu wa fursa za ajira, ukosefu wa usawa pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira. Hapa binadamu awe ni kiini na hatima ya sera na mikakati yote ya shughuli za kiuchumi.

Kardinali Turkson anaendelea kukazia umuhimu wa kuwa na sera makini za kiuchumi zinazosaidia kusimamia na kuratibu mashindano kati ya wadau wa uchumi, rasilimali ya dunia na uwezo wa rasilimali fedha; daima binadamu akiheshimiwa na kuthaminiwa badala ya mwelekeo wa sasa unaokijita katika utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu ndani ya jamii. Kwa namna ya pekee, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanaweza kuwa ni msaada mkubwa katika mchakato wa ujenzi wa uchumi unaojali na kuheshimu utu wa binadamu na mahitaji yake msingi.

Kimsingi, huu ni uchumi ambao unapaswa kupambana na changamoto za ukosefu wa fursa za ajira, wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi pamoja na utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote. Ikumbukwe kwamba, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanajikita katika mshikamano unaosimikwa katika kanuni auni ili kujenga jamii inayowajibika na kusaidiana.

Kardinali Turkson anaendelea kufafanua kwamba, mikopo midogo midogo na yenye masharti nafuu ni nyenzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya balaa la umaskini duniani, kwa kuwajengea wananchi matumaini ya kuweza kuchakarika katika mchakato wa kujijengea uwezo wa kiuchumi. Kwa bahati mbaya, Benki na Taasisi nyingi za fedha duniani zilishindwa kuwekeza matumaini kwa maskini na matokeo yake, watu wengi wanaendelea kutumbukia katika umaskini wa hali na kipato.

Kumbe, mikopo midogo midogo inapaswa kuwa na mwelekeo wa kijamii, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa mshikamano unaoratibiwa na kanuni auni. Wananchi wenye kipato cha chini wanaokopeshwa wanapaswa pia kuheshimu dhamana na wajibu wao kwa kurejesha fedha iliyokopwa, ili kulinda heshima na utu wao kama binadamu! Kwa njia hii, hata maskini wanaweza kuchakarika katika maboresho ya: kazi, makazi na ardhi, kwa kushiriki katika mchakato wa mageuzi katika medani mbali mbali za maisha, kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Mikopo isaidie mchakato wa kukuza maendeleo endelevu na shirikishi kwa watu wote.

Kardinali Peter Turkson anahitimisha hotuba yake kwa kusema kwamba, Kanisa linapenda kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya umaskini duniani na kwamba upendeleo kwa maskini ni moja ya changamoto msingi zinazopaswa kufanyiwa kazi na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kwani ikumbukwe kwamba, Siku ya mwisho, watu watakuhukumiwa kwa jinsi ambavyo wamesaidia kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Umaskini unaweza kupewa kisogo ikiwa kama kutakuwepo na uchumi jamii unaosimikwa katika: usawa na katika miundo mbinu inayolinda na kutetea utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.