2016-10-18 14:43:00

Saidieni mchakato wa mapinduzi ya huruma ya Mungu kwa watu!


Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Yangon nchini Myanmar katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Wakleri nchini humo hivi karibuni, amewataka kuwa ni vyombo, mashuhuda lakini zaidi wanamapinduzi watakaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumwilisha huruma ya Mungu iliyofunuliwa na Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa watu wa mataifa.

Kardinali Bo anasema kutokana na binadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kuendelea kukengeuka kwa kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa maisha na vipaumbele vyake sanjari na kuporomoka kwa maadili na utu wema, kuna haja ya kufanya mapinduzi ya kimaadili kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uwe ni msingi wa mapinduzi ya maisha ya kiroho kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata utimilifu na utakatifu wa maisha kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu.

Kardinali Bo anasema, inasikitisha kuona kwamba, historia ya maisha ya mwanadamu inaendelea siku hadi siku kujikita katika mipasuko, kinzani na vita inayowanufaisha wajanja wachache wanaoendelea kuneemeka kwa damu ya maskini wanaotumbukizwa katika vita na migogoro ya kijamii. Vitendo vya kigaidi na misimamo mikali ya kidini na kiimani ni changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo.

Kila kukicha kuna taarifa za mauaji ya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia kiasi kwamba, watu wengi wanaendelea kujengewa wasi wasi na hofu kuhusu uhakika wa usalama wa maisha yao. Kutokana na hali na mazingira kama haya mapinduzi ya huruma ya Mungu yanakuwa na umuhimu wa pekee kwa walimwengu mamboleo, ili kweli waweze kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma. Itakuwa ni nafasi ya kujenga utamaduni wa haki, amani, upendo, maridhiano na msamaha wa kweli kwa kuachana na tabia ya chuki na hali ya kupenda kulipizana kisasi, bali wajivike fadhila ya msamaha kama Kristo anavyofundisha katika Sala kuu ya Baba Yetu wa mbinguni!

Kardinali Bo anakiri kwamba, dhana ya huruma ya Mungu, upendo na msamaha wa kweli kwa mwanadamu katika ulimwengu mamboleo ni changamoto kubwa, lakini ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini na utambulisho wa utu na heshima ya binadamu inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Muumbaji na Mkombozi. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kushuhudia kwa walimwengu Injili ya huruma ya Mungu kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hawa ndio walengwa haswa wa Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu ameonesha kuwa ni chombo na shuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu kwa maskini, wagonjwa, wafungwa, wakimbizi na wahamiaji; mambao ambayo yako wazi kabisa katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni changamoto pia kwa familia na waamini katika ujumla wao kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, kielelezo makini cha imani tendaji, inayoshuhudiwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Wakleri wawe ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu wanapoadhimisha mafumbo ya Kanisa, lakini zaidi wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho; Sakramenti ambazo ni chemchemi ya huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Mapadre waungamishaji, waoneshe huruma kwa kusamehe dhambi, kwa kuganga na kutibu makovu ya dhambi za binadamu, wakitambua kwamba, hata wao katika maisha na utume wao, wanapaswa kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu katika maisha. Kiti cha maungamo, kitumike kama hospitali ya kutibu majeraha ya dhambi za binadamu.

Kardinali Bo anawapongeza Wakleri na Watawa wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wagonjwa, wazee na watoto; vijana na wote wanaohitaji kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Huu ni ushuhuda wa matendo ya huruma yanayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Lakin matendo ya huruma yawe ni kielelezo pia cha familia za Kikristo kwa kuguswa na mahangaiko ya jirani zao badala ya kuwageuzia kisogo! Kila mwamini ajitahidi kuwa ni msamaria mwema kwa watu wanaoteseka; kiroho na kimwili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.