2016-10-17 15:29:00

Waziri mkuu atema cheche kali mkoani Lindi!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, Bw. Bakari Mohammed kuhakikisha hospitali ya wilaya hiyo inakusanya mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki.  Ametoa agizo hilo Jumapili, Oktoba 16, 2016 wakati alipotembelea hospitali ya wilaya ya Nachingwea akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Lindi. Waziri Mkuu amesema Serikali ilishaagiza taasisi zote za umma kutumia mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato kwa lengo la kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma.  Amesema taasisi ambazo tayari ziameanza kutumia mfuko huo katika ukusanyaji wa mapato zimeweza kuongeza kiwango cha makusanyo kutoka sh. 300,000 hadi milioni nne kwa siku.

Pia aliwaagiza viongozi wa wilaya hiyo kuendelea kuwahamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao utawawezesha kupata huduma ya matibabu bure katika kipindi cha mwaka mzima. Akizungumzia kuhusu matibabu kwa wazee, Waziri Mkuu amemuagiza Bw. Mohammed kuhakikisha anafungua dirisha la kuwahudumia wazee ili kuwarahisishia upatikanaji wa huduma wanapofika hospitalini hapo. “Mkurugenzi hakikisha watendaji wako wa kata na vijiji wamebaini wazee wote katika maeneo yao na kuwatengenezea vitambulisho vitakavyowawezesha kupatibiwa bure,” amesema.

Naye Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dk. Samwel Laizer amesema mwamko mdogo wa jamii kujiunga na CHF ni moja kati ya changamoto zinazowakabili katika utoaji wa huduma za afya. Dk. Laizer amasema kati ya kaya 30,000 zilizoko wilayani Nachingwea ni kaya 7,133 tu ndizo zilizojiunga na mfuko wa CHF.

Awali Waziri Mkuu alizungumza na watumishi wa wilaya hiyo kwenye ukumbi wa Chuo Cha Walimu na kuwataka wabadilike ili waweze kuwatumikia wananchi kwa uadilifu bila ya kujali itikadi zao za kidini na kisiasa. Amesema Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuwatumikia wananchi. “Serikali haitaridhika kuona wananchi wakizagaa kwenye ofisi za halmashauri hiyo bila ya kusikilizwa”,  amesema.

Wakati huo huo, Waziri mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba kuifanyia marekebisho makubwa Bodi ya Korosho na menejimenti yake baada ya kushindwa kusimamia zao hilo ipasavyo. Amesema Serikali itafanya mapitio ya bodi zote za mazao ya biashara na imeanza na zao la korosho kisha zao la pamba, tumbaku, kahawa, katani na chai. Katika tathmini na mapitio hayo, bodi itakayobainika kushindwa kutekeleza majukumu yake itavunjwa.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo Jumapili, Oktoba 16, 2016) wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja cha Sokoine wilayani Nachingwea mkoani Lindi. Alisema anaishangaa bodi hiyo kuacha kutekeleza majukumu yake na kuingilia minada ya korosho na kuzuia baadhi ya wafanyabiashara wasiweze kununua zao hilo hali inayoashiria kuwepo kwa watu waliopangwa kununua bila ya kufuata utaratibu.

“Bodi leo wamejipa jukumu la kusimamia minada ! sio kazi yao ni kazi ya chama kikuu, zao la korosho linalimwa kutoka mkoani Ruvuma hadi Tanga, mtasimamia minada mingapi viachieni vyama vikuu. Vyama vikuu vikiharibu walalamikaji waje kwenu kama sehemu ya rufaa. Sasa nyinyi mnasimamia minada mnaharibu walalamikaji watakwenda kwa nani ? kwa nini mng’ang’anie kwenda kwenye minada,”alihoji Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alisema Ijumaa Oktoba 14,2016) bodi hiyo ilisitisha mnada wa korosho Lindi kwa sababu wanunuzi hawakuweka bondi (dhamana ya mauzo) na alishatoa maagizo ya kuwataka wanunuzi wasiruhusiwe kununua hadi waweke asilimia 25 ya malipo. Alisema maagizo hayo aliyatoa tangu mwezi Aprili ila watendaji wa bodi hiyo hawakuyafanyia kazi kwa wakati na badala yake waliwazuia wafanyabiashara waliotaka kununua korosho Lindi kwa madai ya kutokuwa na bondi huku wakiwaruhusu wa Mtwara.

“Kama kule walinunua bila bondi kwa nini wasiwaruhusu na Lindi wakanunua bila bondi ili nijue kwamba mliamua kugoma kuteleza maelekezo ya Serikali? Au hamkumtaka aliyeshinda nyie mlikuwa mnamtaka nani nitashughulika na nyie,” alisisitiza. Aliongeza kuwa “Nimesema tukitoa maelekezo lazima yatekelezwe na atakayeshindwa hatufai, Mheshimiwa mbunge umelalamika juu ya bodi hawa ndio wabeba maelekezo hatujawahi kuona bodi ya korosho ikienda vijijini kuzungumza na vyama vikuu hata mara moja,”.

Akizungumzia kuhusu suala la wakulima kulazimishwa kufungua akaunti za kupitishia malipo yao alisema wasiwalazimishe.“Waelimisheni wakulima umuhimu wa kufungua akaunti lakini si kwa kuwalazimisha wote wawe na akaunti hadi yule mwenye kilo tano…na akaunti yenyewe inafunguliwa kwa sh. 100,000,”alisema.

Alisema“’wanashindwa kutekeleza niliyowaagiza, halafu wanasingizia utendaji wao mbovu kuwa ndio maagizo yangu,’ niliwaagiza wapi,” alihoji na kuongeza kuwa “yapo makundi yanafanya mambo yanavyotaka alafu yakiwazidi mambo wanasingizia viongozi wajuu na ndio wale wanaosema kila kitu nimeagizwa kutoka juu, juu wapi?  “Lazima tuendelee kudhibiti nidhamu ya vyombo vya tunavyoviunda kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Tutaendelea kusimamia nidhamu kwa taasisi zinazowahudumia wakulima nchi nzima,” alisisitiza.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi alimkabidhi Waziri Mkuu msaada wa sh. milioni 16.3 pamoja na nguo kwa ajili ya kusaidia wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.








All the contents on this site are copyrighted ©.