2016-10-17 08:29:00

Waraka wa Maaskofu Katoliki: Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri


Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri yanayoongozwa na kauli mbiu “Kutoka katika kinzani kuelekea kwenye umoja. Tumeungana katika matumaini” ni muda muafaka wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene; ni kipindi cha kumshukuru Mungu kwa mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika kipindi cha miaka hamsini tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipoanzisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene.

Ni kipindi cha kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu inayowawajibisha kushikamana kwa ajili ya umoja na mshikamano wa familia ya Mungu duniani! Kutokana na umuhimu wa maadhimisho haya, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka katika nchi za Scandinavia limeandika barua ya kichungaji kama sehemu ya kumbu kumbu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri duniani yaliyosababisha mpasuko wa Kanisa pamoja na mahangaiko ya watu hata pengine kwa nyakati hizi.

Maaskofu wanakaza kusema, maadhimisho haya iwe ni fursa ya kufanya toba na wongofu wa ndani kutokana na machungu ambayo yalijitokeza ndani na nje ya Kanisa. Waraka huu wa kichungaji unaongozwa na kauli mbiu “Kutoka katika kinzani kuelekea katika umoja” unalenga kuwachangamotisha Wakristo wa Makanisa haya mawili kuangalia kwa kina na mapana mchakato wa majadiliano ya kiekumene utakaowasaidia kukua kwa pamoja katika imani, matumaini na mapendo.

Maaskofu Katoliki kutoka katika nchi za Scandinavia wanasema, wanapenda kujizatiti katika kukuza na kudumisha mchakato wa haki, amani na upatanisho na waamini wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri, ili hatimaye, waweze kuwa wamoja katika Kristo Yesu. Maaskofu Katoliki wanabainisha mambo msingi ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi mintarafu Mafundisho Tanzu ya Kanisa kama yalivyobainishwa katika Waraka wa pamoja kati ya Wakatoliki na Waluteri kunako mwaka 2013.

Maaskofu wanawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya huko Uswiss kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 1 Novemba 2016. Maaskofu Katoliki kutoka Scandinavia wanahitimisha waraka wao wa kichungaji kwa kukazia kwamba licha ya tofauti zilizopo kati ya Wakatoliki na Waluteri, wana amini kwamba, kwa njia ya neema ya Mungu wanaweza kupata njia itakayowawezesha kujenga tena umoja wa Wakristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.