2016-10-17 14:12:00

Simameni kidete kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kuanzia tarehe 14- 16 Oktoba 2016 amekuwa na ziara ya kikazi nchini Yordan kama mwakilishi maalum wa Baba Mtakatifu Francisko katika uzinduzi rasmi wa Madhabahu ya Ukumbusho wa Musa kwenye Mlima Nebo, mahali ambapo Mwenyezi Mungu alimwonesha Musa nchi ya ahadi, lakini hakubahatika kuingia ndani yake. Madhabahu haya yana utajiri mkubwa katika maisha ya kiroho. Amekutana na kuzungumza na viongozi wa Makanisa na Serikali pamoja na kutembelea miradi ya kijamii inayofadhiliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.

Kardinali Sandri akiwa nchini Yordan ametembelea pia “Bustan ya Huruma ya Mungu” kwa kukutana na kuzungumza na viongozi pamoja na wafanyakazi wanaotekeleza dhamana yao kwenye Kituo cha Bikira Maria Malkia wa Amani, kilichoanzishwa kwa utashi wa Baba Mtakatifu Francisko kutokana na fedha iliyokusanywa wakati wa Onesho la Chakula Duniani, Expo 2015, mjini Milano, Italia.

Amekutana na kuzungumza na vijana wanaohudumiwa na Shirika la Wafranciskani huko Jabal Al Webdeh pamoja na kuwatembelea wagonjwa wanaohudumiwa kwenye Hospitali iliyoko Misdar, mahali ambapo familia kutoka Syria zinahudumiwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Yordan, yaani “Caritas Jordan” kama kielelezo cha mshikamano wa huruma na mapendo kwa watu wanaoteseka kutoka na vita inayoendelea huko nchini Syria.

Kardinali Sandri katika Ibada ya kuzindua Madhabahu ya Ukumbusho wa Musa kwenye Mlima Nebo kwa kutabaruku Altare yake, amewashukuru wale wote waliojisadaka kwa ajili ya kufanikisha ukarabati huu ambao utawawezesha waamini kumwimbia Mungu utenzi wa shukrani, sifa na utukufu, huku wakiwa wameungana na Jeshi kubwa la watakatifu mbinguni, licha ya utengano wa Kanisa ambao bado unaendelea kulitesa Kanisa la Kristo. Eneo hili ni kumbu kumbu ya waamini wanaokumbuka matendo makuu ya Mungu katika historia ya ukombozi.

Hapa ni mahali ambapo Musa aliweza kuonana uso kwa uso na Mwenyezi Mungu, kiasi cha kuogopa na kuufunika uso wake, changamoto kwa waamini kujenga utamaduni wa kujadiliana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu, ili kujenga imani kwa Mwenyezi Mungu. Licha ya Musa kuwaongoza Waisraeli kwa mkono wenye nguvu lakini hakuweza kuingia kwenye Nchi ya ahadi kutokana na kuwa na moyo mgumu, changamoto ya kutubu na kumwongokea Mungu, ili hatimaye, kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano.

Huu ni mwaliko kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kutetea maisha ya watu wasiokuwa na hatia wanaoendelea kufa kutokana na vita, dhuluma, nyanyaso na misimamo mikali ya kidini. Watu wajifunze kumwachia Mungu nafasi katika maisha yao kwa kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Ni matumaini ya Kardinali Sandri kwamba, Madhabahu ya Ukumbusho wa Musa yatakuwa ni mahali patakatifu kwa waamini kuweza kujichotea neema na baraka hasa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Waamini wanakumbushwa kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka ni mshindi dhidi ya dhambi na mauti, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwinua macho ya imani, matumaini na mapendo. Kwa njia ya Musa, waamini wamemtambua Mungu kuwa kweli Mungu ni chemchemi ya maisha na Bwana wa historia. Madhabahu haya yawe ni mahali pa kukutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu, ili kuonja na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu inayofunika uzito wa dhambi na mauti. Vijana wa kizazi kipya wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani, upendo na mshikamano, daima wakitafuta mafao ya wengi, uhuru, haki na upatanisho. Ni kipindi muafaka kwa Makanisa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kujenga umoja wa Kanisa la Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.