2016-10-16 08:32:00

Watakatifu wapya walikuwa ni watu wa sala, wakarimu na waaminifu


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 16 Oktoba 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwatangaza wenye heri saba kuwa watakatifu, Ibada ambayo imehudhuriwa na bahari ya watu kutoka ndani na nje ya Italia. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amewaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaumbia moyo safi, moyo wenye ukarimu na mwaminifu, ili waweze kumtumikia Mwenyezi Mungu katika ukweli na usafi wa moyo.

Waamini wanatambua kwamba, kwa nguvu zao peke yao hawawezi kufanikisha azma hii ndiyo maana wanamkimbilia Mungu kwa njia ya sala kama zawadi, changamoto hata kwa waamini waliokuwa wamefurika katika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kushuhudia baadhi ya Wenyeheri wakitangazwa kuwa watakatifu. Hawa ni watu waliofikia hatima ya maisha yao, kwa kuwa na moyo wa ukarimu na mwaminifu; mambo ambayo walikirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala. Hawa ni watu anasema Baba Mtakatifu waliosali kwa nguvu zao zote, wakapambana kufa na kupona hatimaye wakashinda pamoja na Kristo Yesu.

Waamini wanahamasishwa kusali kama alivyofanya Musa, aliyekuwa ni mtu wa Mungu na mtu wa sala, ili kuweza kushinda pambano katika maisha, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli walivyokuwa wanapambana na Waamaleki na kushinda vita kwa nguvu ya sala. Baba Mtakatifu anawataka waamini kujikita katika mapambano ya sala si kwa ajili ya kushinda vita, bali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, amani inashinda na kutawala katika maisha ya watu, kwa kushikamana na kusaidiana kama ilivyokuwa kwa Haruni na Huri kwa Musa, ili kumwezesha Mwenyezi Mungu kuhitimisha kazi yake anayokusudia katika maisha ya binadamu!

Baba Mtakatifu anawataka waamini pia kuendelea kuwa imara na thabiti katika imani, kwa kuwa wadumifu katika maisha ya sala kama ambavyo Mtakatifu Petro anavyomhimiza Mtakatifu Timoteo, dhana inayokaziwa pia na Kristo Yesu katika Injili, akiwataka wafuasi wake kusali bila kuchoka, ili kuwa imara na thabiti katika imani na ushuhuda wa Kikristo wenye mvuto na mashiko.

Kuchoka na kukata tamaa katika maisha ni sehemu ya ubinadamu, lakini waamini wanapaswa kutambua kwamba, wao ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa; Kanisa ambalo linainua mikono yake mbinguni usiku na mchana ili kumwimbia sifa Kristo Mfufuka pamoja na Roho wake Mtakatifu. Ni kwa njia ya Kanisa peke yake pamoja na kujikita katika sala ya Kanisa, waamini wanaweza kubaki waaminifu na kuendelea kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Yesu anawajuza wafuasi wake kwamba atawatendea haki kwa wakati muafaka, lakini hawana budi kuendelea kupiga kelele kwa njia ya sala bila ya kukimbia na kujificha katika utupu na ubinafsi, kwani kusali ni mapambano yanayomshirikisha pia Roho Mtakatifu anayewafundisha, kuwaongoza na kuwawezesha kusali kama watoto wa Baba! Ikumbukwe kwamba, watakatifu ni watu ambao wamezama kabisa katika Fumbo la Sala, watu wanaopambana kufa na kupona kwa njia ya sala; kwa kumwachia Roho Mtakatifu anayepambana pamoja nao hadi mwisho.

Watakatifu saba waliotangazwa na Mama Kanisa walipigana vita vitakatifu vya imani na mapendo kwa njia ya sala, wakabahatika kuwa imara na thabiti katika imani, huku wakiwa na mioyo yenye ukarimu na aminifu. Kwa njia ya mifano na maombezi ya watakatifu hawa, Mwenyezi Mungu pia awajalie waamini kuwa kweli ni watu wa sala wanaomlilia Mungu usiku na mchana bila kuchoka, pamoja na kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuambatana pamoja nao katika sala, huku wakisaidiana na kuhimizana katika sala, ili kweli huruma ya Mungu iweze kushinda na kutawala kati ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.