2016-10-16 10:49:00

Simameni kidete kupambana na umaskini duniani!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 16 Oktoba 2016 kwa ajili ya kuwatangaza watakatifu wapya saba waliosali kwa nguvu zao zote, wakapambana kufa na kupona na hatimaye wakashinda, amewashukuru  waamini na watu kutoka katika mataifa mbali mbali waliohudhuria Ibada ya kuwatangaza watakatifu wapya. Kwa namna ya pekee, amewakumbuka wawakilishi wa Serikali kutoka Argentina, ujumbe ambao umeongozwa na Rais Mauricio Macri wa Argentina aliyekuwa amefuatana na kundi la watu 20.

Ujumbe kutoka Hispania uliokuwa na watu 9 umeongozwa na Bwana Jorge Fernàndes Dias, Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi. Ujumbe wa Ufaransa ulikuwa na jumla ya watu 11 na umeongozwa na  Bi Segolène Royal, Waziri wa Mazingira. Ujumbe kutoka Mexico ulikuwa na mtu mmoja na ameongozwa na Dr. Herrera Mena, Mkurugenzi mkuu mwambata wa masuala ya kidini nchini Mexico. Mwishoni, Bi Maria Elena Boschi, Waziri wa Mabadiliko ya Katiba na Uhusiano na Bunge kutoka Italia, ameongoza ujumbe wa watu 5 kutoka Italia katika Ibada hii.

Baba Mtakatifu amewataka waamini kwa njia ya mifano na maombezi yao, waweze kuwasaidia kuwa kweli mashuhuda amini na angavu katika nyajibu na dhamana walizokabidhiwa kwa ajili ya huduma na ustawi wa Kanisa na Jamii inayowazunguka. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa amekumbusha kwamba, Jumatatu tarehe 17 Oktoba 2016 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kupambana na Umaskini Duniani.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuunganisha nguvu zao za kimaadili na kiuchumi katika mapambano dhidi ya umaskini unaoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu, kwa kujikita katika sera makini zinazosimamia tunu msingi za kifamilia pamoja na kazi pamoja na kujikita katika sala kwa ajili ya kuombea amani, chini ya ulinzi na tunza na Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.