2016-10-15 09:50:00

Papa Francisko aomboleza kifo cha Mfalme Bhumibol wa Thailand!


Familia ya Mungu nchini Thailand inaomboleza kifo cha Mfalme Bhumibol Adulyadej kilichotokea hivi karibuni na kwamba, maombolezo haya yatadumu kwa kipindi cha mwaka mzima, ili kuonesha ni kwa jinsi gani Thailand imempoteza kiongozi wake mashuhuri aliyeongoza kwa takribani miaka 70 kama Mfalme. Mtoto wake wa kiume Maha Vjiralonkorn mwenye umri wa miaka 64 ndiye atakayerithi kiti cha kifalme cha baba yake.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam za rambi rambi alizomtumia Waziri mkuu wa Thailand, Jenerali Prayuth Chan-ocha ameonesha masikitiko yake kutokana na kifo cha Mfalme wao na kumwomba aweze kufikisha salam zake za rambi rambi kwa familia ya marehemu pamoja na wananchi wote wa Thailand ambao wameguswa kwa uchungu mkubwa na msiba huu. Anasikitika kwa kuondokewa na kiongozi aliyeacha urithi mkubwa wa hekima, nguvu na uaminifu.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wananchi wa Thailand wataweza kushikamana katika kipindi hiki kigumu na kuendelea kufanya kazi kwa umoja ili kukuza na kudumisha misingi ya amani na mshikamano. Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa wote walioguswa na msiba huu mzito! Mfalme Bhumibol Adulyadej ni kati ya nguzo kuu za umoja na mshikamano wa kitaifa nchini Thailand. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, hali ya mfalme ilianza kuteleleka na kudhohofu kiasi cha kuwafanya baadhi ya wananchi kutumia mwanya huu kuvuruga misingi ya haki, amani na maridhiano nchini humo, mambo ambayo yamepelekea majaribio mawili ya kutaka kuipindua Serikali halali iliyoko madarakani na vifo vya watu wengi wasiokuwa na hatia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.