2016-10-14 14:50:00

Iweni na ujasiri wa kiimani!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi, tarehe 13 Oktoba 2016 amehitimisha hija yake ya kitume nchini Ureno aliyoianza hapo tarehe 11 Oktoba 2016 kwa kuzungumzia kuhusu utambulisho wa wananchi wa Jumuiya ya Ulaya unaojikita katika misingi ya Ukristo; umuhimu wa kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa ujasiri, ari na moyo mkuu pamoja na kuwataka waamini kujifunza kutoka katika shule ya Moyo Safi wa Bikira Maria, ili waweze kuwa na ujasiri wa kuweza kukabiliana na Misalaba ya Maisha yao: kiroho na kimwili! Alipata nafasi pia ya kukutana na kuzungumza na Waziri mkuu wa Ureno Dr. Antònio Costa.

Kardinali Parolin katika mahubiri yake baada ya tafakari ya kina ya Ibada ya Rozari Takatifu, muhtasari wa historia ya huruma ya Mungu kwa binadamu, Siku ya Alhamisi tarehe 13 Oktoba 2016 asubuhi, alikazia umuhimu wa kumjifunza Bikira Maria, ili kuwa na ujasiri wa kukabiliana na Misalaba ya maisha kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria aliyesimama chini ya Msalaba na kushuhudia Mwanaye mpendwa Yesu Kristo akiinamisha kichwa na kukata roho!

Bikira Maria alionesha imani, matumaini na mapendo, akajiachilia mikononi mwa Mungu bila kukatishwa tamaa na wakuu wa nchi na askari! Itakumbukwa kwamba, wakati ule haikuwa rahisi kuwakaribia watu waliokuwa wamehukumiwa kifo! Lakini Bikira Maria akapita lile pazia la chuma hata kudiriki kusimama chini ya Msalaba, kielelezo makini cha hekima, huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu!

Kardinali Parolin katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, nchini Ureno, Jumatano jioni tarehe 12 Oktoba 2016 aliwataka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza katika majiundo ya kiimani, ili kuweza kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Kristo Yesu kwa moyo na akili yote. Amewataka waamini kutofautisha habari na mafundisho tanzu ya Kanisa. Ulimwengu mamboleo umezungukwa na vyombo vingi vya mawasiliano ya kijamii vinavyojitahidi kuwahabarisha watu mambo mbali mbali yanayoendelea kujiri duniani. Mwanadamu katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia anao uwezo wa kupata habari nyingi, hali inayomwezesha raia kuwa na ufahamu wa mambo msingi yanayomwajibisha kushiriki kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya jamii inayomzunguka; kwa kutambua na kuthamini haki na wajibu wake katika mchakato mzima wa maisha ya kijamii!

Kardinali Parolin, anawataka waamini kutambua kwamba, si wingi wa habari kuhusu Mwenyezi Mungu na Mwanaye mpendwa Yesu Kristo zinazowafanya kuwa wachamungu; bali ni imani yao kwa Kristo Yesu aliyezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu; imani inayozamishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Waamini wanapaswa kujenga utamaduni wa kusikiliza na kulitafakari Neno la Mungu kwa makini, ili kuliachia nafasi liweze kuwafunda na kuwaunda, tayari kuwa ni mitume waamini na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa kumwachia nafasi Kristo Yesu, ili aweze kuwa ni Bwana na Mwalimu wao wa maisha.

Kardinali Pietro Parolin, kabla ya Ibada ya Misa Takatifu, alipata nafasi ya kuzungumza na mahujaji waliofika mjini Fatima kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria, kujitahidi kumjifunza Kristo kwa njia ya Bikira Maria, daima wakiwa na kiu ya kutaka kukutana na Kristo Yesu anayezima kiu ya maisha yao ya ndani. Waamini wajitahidi kudumisha moyo safi kama alivyokuwa Bikira Maria na huo ndio moyo wa Kanisa la Kristo! Kardinali alishiriki katika Ibada ya Kubariki Mishumaa na baadaye kuongoza maandamano ya Ibada ya Rozari Takatifu yaliyohitimishwa kwa Baraka ya Sakramenti kuu; tukio lililohudhuriwa na umati mkubwa wa mahujaji wagonjwa, wanaokimbilia tunza na ulinzi wa Bikira Maria katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.