2016-10-14 10:17:00

Changamoto ya wakimbizi na wahamiaji waathirika wakuu ni watoto wadogo!


Takwimu zinaonesha kwamba, nusu ya wakimbizi na wahamiaji wote ni duniani ni watoto wenye umri chini ya miaka 18 na kwamba, kuna zaidi ya watoto millioni 50 wanaoishi kama wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Watoto zaidi ya millioni 20 wamelazimika kuishi kama wakimbizi na wahamiaji kutokana na vita inayoendelea kupamba moto sehemu mbali mbali za dunia. Kati ya watoto mia mbili duniani, mmoja wao anaishi kama mkimbizi na mhamiaji!

Hizi ni takwimu zinazoacha simanzi na uchungu moyoni mwa wapenda amani, ustawi na maendeleo ya watoto duniani zilizotolewa Alhamisi, tarehe 13 Oktoba 2016 na Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa la Shughuli za Kichungaji kwa ajili ya Wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, wakati akiwasilisha Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya 103 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani itakayoadhimishwa Jumapili, tarehe 15 Januari 2017. Ujumbe huu unaongozwa na kauli mbiu “Wahamiaji wadogo ni wahanga pasi na sauti”.

Watoto ndio wanaoathirika zaidi kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, kiasi kwamba, wanajikuta wakiwa wametumbukizwa katika: utumwa mamboleo, biashara haramu ya binadamu na dawa za kulevya; vita pamoja na magenge ya kihakifu; mambo yanayonyanyasa na kudhalilisha utu, heshima na haki za watoto hawa. Hizi ni sababu msingi kabisa zilizompelekea Baba Mtakatifu Francisko kuamua kuelekeza jicho lake lenye huruma kwa ajili ya hatima ya maisha ya watoto ambao wanajikuta wakiwa ni wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Vegliò anasema, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto kubwa ya kimataifa inayowagusa kwa namna ya pekee, watoto na vijana wanaolazimika kuzikimbia familia na nchi zao na hivyo kujikuta wakiwa wamebeba ndani mwao mzigo mkubwa wa madonda katika maisha na makuzi yao. Ni watu wanaotamani: usalama, amani na maisha bora zaidi. Kundi kubwa la watoto na vijana hawa ni wale wanaotembea peke yao bila ya tunza na uangalizi kutoka kwa wazazi na walezi wao.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2015 kulikuwa na watoto wakimbizi na wahamiaji zaidi ya laki moja waliokuwa peke yao bila ya ulinzi wala tunza ya wazazi na walezi wao, wanaoomba hifadhi ya kisiasa katika nchi 78 duniani. Hii ni idadi kubwa sana ya watoto kuwahi kuomba hifadhi ya kisiasa duniani kutokana na kulazimika kuzikimbia nchi zao. Asilimia 50% ya idadi ya watoto wote hawa hawakupata fursa ya masomo ya shule ya msingi. Asilimia 22% ya watoto hawa walibahatika walau kusoma shule za sekondari na kwamba ni asilimia 1% ya watoto hawa wanaoweza kupata bahati ya kuendelea na masomo kwenye vyuo vya elimu ya juu na vyuo vikuu.

Kardinali Vegliò anakaza kusema, wengi wa wakimbizi hawa ni wale wanaolazimika kuzihama nchi zao kutokana na vita, dhuluma, nyanyaso na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Watoto kutoka Syria ni mfano wa changamoto hii. Asilimia 80% ya watoto waliozaliwa wakati wa vita huko Syria, haijulikani na wala hawana nyaraka zinazowawezesha kupata haki ya uraia, elimu na afya. Hili ni kundi la watoto linaloishi katika ombwe na utupu!

Watoto hawa wanakabiliwa na majanga mbali mbali katika maisha yao kwani kwanza kabisa ni watoto wadogo hawawezi kujitetea; Pili ni wageni, wahamiaji na wakimbizi; Na tatu hawana haki kiasi kwamba, wanashindwa kuomba hifadhi ya kisiasa. Leo hii kuna kundi kubwa la watoto wasiokuwa na tunza wala hifadhi ya wazazi na walezi wao wanaoomba hifadhi ya kisiasa katika Nchi zilizoendelea zaidi duniani Katika kipindi cha mwaka 2015 zaidi ya watoto elfu kumi waliowasili Barani Ulaya bila tunza na ulinzi wa wazazi na walezi wao wamepotea na wala hawajulikani mahali walipo, hali inayoonesha wasi wasi kwa ajili ya hatima, ustawi na maendeleo ya watoto hawa kwa siku za usoni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.