2016-10-13 15:40:00

Papa Francisko akutana na kundi la mahujaji Waluteri


Baba Mtakatifu Francisko majira ya saa tano za asubuhi Alhamisi 13 Oktoba 2016, kwa furaha na shukurani kwa mwenyezi Mungu , alikipokea kikundi cha mahujaji Waluteri kilichoanza  hija  yake Ujeruman, nchi ya mwanzilishi wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri.

Katika hotuba yake  Papa alimshukuru Mwenyezi Mungu , kwa majaliwa yake yanayowawezesha sasa Walutheri na Wakatoliki, kutembea katika njia moja yenye kuwatoa katika marumbano na migogoro kinzani katika ujenzi wa umoja wa wafuasi wa Kristo. Baba Mtakatifu alitaja uwepo huu katika ukumbi wa Paulo wa VI mjini Vatican, ambamo amekutana nao,  tayari ni sehemu muhimu katika kutembea pamoja kama wafuasi wa Kristo. Na kwamba katika kutembea pamoja wanaendelea kupata uzoefu katika  maisha haya mchanganyiko, na hasa katika yale yanayoendelea kuwatenganisha  waamini wa Kristo. Lakini pia akataja kwamba, pia kuna sababu ya kufurahia ya udugu ambao tayari umekwisha kupatikana. Papa ameutaja uwepo wao mbele yake ni dalili ya wazi ya udugu huu. Hivyo Papa alionyesha matumaini yake kwamba udugu huu utandelea kuleta maelewano na kuzidi  kuimarika zaidi na zaidi.

Papa Francisko alieleza na kunukuu kutoka maneno ya Mtume Paulo , ambaye alisema kwamba, kwa njia ya ubatizo walioupokea , wote wanaunda Mwili mmoja wa Kristo, licha ya kuwa makanisa mbalimbali, lakini wote ni mwili mmoja tu.  Na hivyo kama mmoja anateseka wote wanateseka na mmoja wao akifurahi wote kwa pamoja wanafurahi ( 1Kor 12.12-26). Kwa maana hiyo, Papa Francisko amesema , wanaweza kuendelea kutembea pamoja kwa kujiamini katika safari ya kiekumeni, wakiwa wamejawa na utambuzi kwamba, licha ya uwepo bado hoja nyingi zinazowatenganisha,  tayari wako katika umoja. Na yale yanayowaunganisha ni muhimu na mengi zaidi ya yale yanayowatenganisha.

Papa alieleza na kutaja kwamba, mwishoni mwa mwezi huu Oktoba , Mungu akipenda anakwenda Lund, Sweden, kuungana na  Dunia ya Waluteri, kwa madhumuni ya kuadhimisha Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri na huo ukawa ni mwanzo wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri.  Na pia kumshukuru Bwana kwa kupita  miaka hamsini ya mazungumzo rasmi kati ya Walutheri na Wakatoliki, yanayolenga kurejesha umoja kati ya makanisa haya. Papa ameitaja ziara yake kuwa na sehemu muhimu katika maadhimisho  haya , na hasa katika kurejesha angalisho makini katika mwelekeo huu wa umoja kwa siku zijazo, katika mtazamo wa ushuhuda wa kawaida wa maisha ya Kikristo katika dunia ya leo, ambayo ina kiu kali ya  Mungu na huruma yake.  

Papa alieleza na kutaja jinsi dunia inavyotarajio kuona ushuhuda kutoka kwa  Wakristo wenyewe na hasa katika kuifanya huruma ya Mungu ionekane kwa watu wa mataifa kwa njia ya huduma  kwa maskini, wagonjwa, wale ambao wameacha nchi yao kutafuta maisha bora ya baadaye katika nchi zinazojulikana kama ni nchi za Kikristo . Na hivyo watu hao wanatazamia kuuona umoja wa wafuasi wa Kristo, kupitia  huduma na utumishi wao kwa maskini zaidi, na hasa kuiona huruma ya Mungu inayowaunganisha.

Papa kisha alitoa himizo kwa wapendwa  vijana,kuwa daima mashahidi wa huruma, wakati Wanataalimungu wanapoendelea na mazungumzo yao juu ya mafundisho ya Kanisa. Papa aliwataka vijana waendelee kutafiti  kwa bidii fursa ya kukutana kwa ajili ya kupata uelewa zaidi na kusali pamoja na kusaidiana mmoja kwa mwingine, yale mmoja anayopungukiwa.  Kwa nanmna hiyo inakuwa ni utendaji wa wazi na huru ulionje ya fitina na chuki ,bali ni utendaji unaotokana na kuiamini Injili ya  Yesu Kristo, inayotangaza  amani na maridhiano, wao wakiwa kama watendaji wakuu katika uchukuaji wa hatua mpya, katika safari hii inayoelekea katika umoja kamili kwa msaada wake Mungu.  Baba Mtakatifu alieleza na kuwahakikishia kwamba kiroho yuko pamoja nao na akaomba pia wamkumbuke katika sala zao, kwa kuwa anahitaji sana maombi yao . 








All the contents on this site are copyrighted ©.