2016-10-13 11:03:00

Imani yenu iwasaidie kufunua huruma ya Mungu kwa waja wake!


Katika jamii ya leo ambayo inapambwa na matukio ya mateso na ya kukatisha tamaa imani yetu inajaribiwa sana. Uwepo wa vita, udhalimu, unyanyasaji wa ubinadamu ambao unatendwa kila kukicha katika ulimwengu huu kunatuacha na maswali mengi na hata wengine tunadiriki kujiuliza je, Mungu yupo? Je, Mungu ana nguvu na uwezo kama tunavyomfahamu? Kama kweli Mungu yupo na ana uwezo mkuu ni vipi basi aruhusu mwanadamu kubaki katika hali ya mateso?

Lakini tunapolitafakari kwa undani fumbo la umwilisho tunauona ukamilifu wa uwepo na ukaribu wa Mungu kati yetu sisi wanadamu. Mwana wa Mungu, nafsi ya pili katika Utatu Mtakatifu, Bwana wetu Yesu Kristo anakuwa Emmanueli yaani ni Mungu pamoja nasi. Hiki ni kitendo ambacho kinatuonesha katika namna ya juu kabisa ufunuo wa huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu. Mungu anaamua kuichukua namna yetu, kuhisi mateso yetu na kuishi katika mazingira yetu ili mwishoni atufikishe katika utukufu wake (Rejea Flp 2: 6-11).

Ni nini kinapaswa kuwa wajibu wetu sasa kama wanadamu mbele ya Mungu? Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatupatia jawabu. Mwanadamu anapaswa daima kuufanya hai uwepo wa Mungu. Injili ya leo inahitimisha kwa kuweka wazi uhakika wa upendo huo wa Mungu kwetu. “Na Mungu, je! hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia atawapatia haki upesi? Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ni Mungu kweli na mtu kweli anaweka uthibitisho huo: “atawapatia haki upesi”. Maneno haya machache ni faraja na nguvu tunayoipata kutoka kwake Yeye ambaye yu kama sisi na uthibitisho wa ukaribu wa huruma ya Mungu kwetu.

Injili ya leo inaendelea kutupatia changamoto tukiulizwa swali: “walakini atakapokuja Mwana wa Adamu, Je! ataiona imani duniani?. Neno kubwa hapa linaloonekana ni paji la imani ambalo ndilo chanzo cha ukubali wetu kwa uwepo wa Mungu kwetu. Katika somo la kwanza tumeona jinsi wana wa Israeli walivyoonesha imani yao kubwa kwa Mungu na akawapiginia na kushinda. Fimbo ile ya Musa ilikuwa ni ishara ya nguvu ya Mungu na daima ilipoinuliwa juu walishinda na pindi iliposhushwa walielemewa na adui zao. Hili ni himizo kwa uimara wa kiimani, yaani kuwa na imani thabiti daima kwa Mungu. Imani ni karama ambayo inapaswa daima kuchochewa kwani kwa njia yake ndipo tunaweza kumpatia Mwenyezi Mungu nafasi yake na picha inayostahili. Hofu na mashaka ya mwanadamu na hata kutoona nafasi ya Mungu au uwepo wa Mungu mara nyingi huchagizwa na uhaba katika imani: pale mmoja anaposhindwa kumtambua Mwenyezi Mungu, uwezo wake na hata wakati mwingine kushindwa kuzipatia njia zake nafasi ya kwanza.

Mara nyingi mwanadamu amekuwa anasongwa na udhaifu wake na kujikuta fimbo yake inashushwa chini. Hii inaweza kuwa ni katika mazingira yanayomzunguka, mazingira mbayo hayampatii nafasi ya kuiona huruma ya Mungu au inaweza kuwa ni kutoka ndani mwake mwenyewe kwa kuruhusu hofu za kidunia zimtawale huku akisahau hadhi yake kubwa ambayo anavikwa kwa njia ya Kristo. Mwanadamu wa leo amekuwa anaruhusu sana sauti kutoka nje, kutoka kwa wanadamu wenzake zimtawale na si neno la Mungu. Tunashuhudia leo hii kukosekana kwa uimara katika familia mbalimbali, talaka zinatawala ndoa mbalimbali.

Tunashuhudia leo hii ukosefu wa amani kati ya wanadamu licha ya juhudi mazungumzo mengi kufanyika. Tunashuhudia leo hii ubadhirifu, unyanyanyasaji na unyonyaji baina ya wanadamu pamoja na kwamba zipo taasisi na vyombo vingi vya kitaifa, kikanda hata kidunia vinavyoundwa ili kutetea ubinadamu. Zote hizi ni dalili ya kwamba fimbo yetu ya imani imeshushwa chini, hatuwezi kumwona Mungu na mara nyingi matokeo yake tunahangaika kujikwamua bila mafanikio.

Wosia wa Mtume Paulo kwa Timotheo ni urejesho kwetu katika ahadi za Mungu ambazo zinatufikia kupitia Neno lake ambalo ni andiko lenye pumzi ya Mungu. “Wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu”.  Tunaishi katika jamii ambayo inatafuta huria wa taarifa na hivyo kutuweka katika mafundisho mengi ambayo mwisho wake hutufanya kuchanganyikiwa.

Dominika hii ya leo sisi kama Wakristo tunaelekezwa katika kisima msingi cha kuchota taarifa zetu na kutafuta masuluhisho ya changamoto za kiimani. Hili ni Neno la Mungu ambalo ni pumzi yake Mungu, ambalo ni uthibitisho wa uwepo wake kati yetu. Tunapotetereka katika imani yetu na kuanza kutazama pembeni mithili ya mtume Petro alipoitwa na Kristo kutembea juu ya maji huwa tunakutana na vitisho vya upepo na giza kubwa na kujikuta tunazama.

Mtume Paulo anamalizia akituambia: “lihubiri neno, uwe tayari wakati ufaao na wakati usiofaa, karipia, kemea na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho”. Huu ni mwaliko wa uhifadhi Neno la Mungu na kulifikisha mahali popote linapohitajika katika ukamilifu wote. Hapa tunagutushwa katika ushawishi wa kidunia ambao hutupeleka katika kutafuta namna fulani fulani za kulainisha maisha si kama lisemavyo Neno la Mungu bali kama sisi katika ubinadamu wetu tunavyovutika. Hii ndiyo changamoto kubwa ya ulimwengu wetu wa leo ambao daima hutafuta kumpatia mwanadamu raha za kidunia hata kama zinapingana na Neno la Mungu. Tunajikuta tunaruhusu ubinadamu wetu kututawala na kuishusha fimbo yetu ya imani chini.

Mzaburi anatualika kwa maneno mazuri kabisa akisema: “Nitayainua macho yangu niitazame milima; Msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu u katika Bwana, aliyezifanya mbingu na nchi”. Mwaliko huu ni maelekezo ya njia pekee ya kuifuata ili kumkomboa mwanadamu kutoka misiba ambayo inamsonga. Huu ni mwaliko ambao kwa nafasi ya kwanza unaturudisha katika hadhi yetu ambayo tumeipokea tangu uumbaji, kufanana na kuwa mfano wa Mungu.

Dhambi ya Asili ilimjeruhi mwanadamu na hivyo kumdhoofisha katika kuitambua na kuifanya hai chapa hii ya Mungu ndani mwetu ambayo ni uthibisho wa uwepo wake kwetu wakati wote. Lakini katika namna iliyo njema kabisa tumerudishiwa hadhi hiyo na nguvu hiyo kwa njia ya ukombozi wa Bwana wetu Yesu Kristo. Uwezo huo wa kuiinua fimbo yetu ya imani tunao hivyo tuikaribishe neema ya Mungu ili tubaki imara katika imani.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.