2016-10-12 07:26:00

Yaliyojiri wakati wa hija ya Papa Francisko huko Georgia na Azerbaigian!


Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema, hija ya 16 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Georgia na Azerbaijan kuanzia tarehe 30 Septemba hadi tarehe 2Oktoba, iliyoongozwa na kauli mbiu “Sisi sote ni ndugu” ilifunikwa kwa kiasi kikubwa na udugu pamoja na ukarimu. Ni hija ambayo inaendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene katika nchi hizi mbili, ili kukuza na kudumisha umoja, upendo, udugu, haki na amani, kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi.

Katika mahojiano maalum na Gazeti la “L’Osservatore Romano”, Kardinali Koch anasema, viongozi wa Makanisa katika nchi hizi mbili wameonesha kwa namna ya pekee umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya kiekumene; mambo ambayo yanajikita katika uhalisia wa maisha! Viongozi wa Makanisa walimpokea na kumsindikiza Baba Mtakatifu Francisko alipowasili na kuondoka katika nchi hizi mbili hali inayoonesha ukarimu unaopaswa kusimikwa katika maisha ya Kikristo.

Baba Mtakatifu alipokuwa anarejea mjini Roma, alisema, alifurahishwa sana na mapokezi pamoja na ukarimu ulioneshwa na viongozi wa Kanisa wakati wa hija yake ya kitume. Bado kuna changamoto nyingi zinazopaswa kufanyiwa kazi na Makanisa haya mawili anasema Kardinali Koch. Kwa mfano wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko huko Georgia, hakukuwepo na wawakilishi wala ujumbe kutoka katika Kanisa la Kiorthodox la Georgia.

Lakini, mapungufu haya machache, hayawezi kupunguza uzito uliooneshwa na familia ya Mungu nchini Georgia wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko. Mahusiano ya kidugu na Kikristo yataendelea kuimarishwa kati ya waamini wa Makanisa haya mawili kama sehemu ya mchakato wa umoja na mshikamano wa ushuhuda wa Kikristo!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume, aliwataka viongozi wa Makanisa kuwaachia wataalamu wa kitaalimungu kuendeleza majadiliano mintarafu Mafundisho tanzu ya Kanisa, lakini Wakristo wote washikamane katika sala na matendo ya huruma kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Hii inatokana na ukweli anasema Kardinali Koch kwamba, majadiliano ya kiekumene yanayofanywa na watalaam wa Makanisa haya yanalenga pamoja na mambo mengine kutoa ufumbuzi wa kina wa mambo yanayoligawa Kanisa la Kristo, lakini hii ni sehemu tu ya mchakato mzima wa majadiliano ya kiekumene yanayofanywa na Makanisa tangu baada ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anakazia Uekumene wa sala; Uekumene wa huduma ya upendo unaowawezesha waamini wa Makanisa mbali mbali kuweza kufahamiana, kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na umoja, mambo msingi katika kusukuma mbele mchakato wa maendeleo ya binadamu kiroho na kimwili. Kuna Uekumene wa kitamaduni na kisanaa unaojikita katika masuala ya kidini bila kusahau Uekumene wa damu unaofumbatwa katika ushuhuda kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiini na msingi wa imani ya Kikristo! Uekumene unapaswa kusimikwa katika uhalisia wa maisha ya waamini.

Baba Mtakatifu anatambua fika changamoto zilizopo katika kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene na Makanisa ya Kiorthodox mintarafu Mafundisho tanzu ya Kanisa, lakini hata hivyo, bado anaendelea kuhimiza: umoja, mshikamano na upendo kati ya Wakristo. Utengano miongoni mwa Wakristo ni tukio la kihistoria ambalo linapaswa pia kufanyiwa kazi katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kuishi na kushirikiana katika upendo.

Wakristo watambue machungu yanayosababishwa na utengano, kwani wote kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanajenga Kanisa la Kristo, kumbe majadiliano ya kiekumene ni muhimu katika kukuza na kudumisha umoja wa Makanisa! Kardinali Koch anakaza kusema, jitihada za Baba Mtakatifu Francisko katika kudumisha mchakato wa kiekumene zinamwilishwa katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa ndiyo maana hivi karibuni amekutana, amezungumza na kusali na wajumbe wa  Kanisa la Kiinjili la Kiluteri wakati alipokuwa mjini Assisi pamoja na kusali na ujumbe wa Kanisa Anglikani, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu mchakato wa majadiliano ya kiekumene ulipoanzishwa kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa Anglikani.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni tukio ambalo pia limepambwa kwa namna ya pekee na matukio makubwa ya kiekumene. Baba Mtakatifu tarehe 12 Februari 2016 amebahatika kukutana na kuzungumza na Patriaki mkuu wa Moscow na Russia nzima Kirill, mjini Havana, Cuba. Tarehe 16 Aprili 2016 akiwa mjini Lesvos, Ugiriki alikutana na kuzungumza na Patriaki Bartolomeo wa kwanza pamoja na Patriaki Hieronymos, ili kuonesha umoja na mshikamano wa Makanisa katika kukabiliana na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi duniani wakati huu.

Kimsingi, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa majadiliano ya kiekumene, ili wote wawe wamoja! Umoja wa wakristo si tukio la muujiza, bali ni hija inayofanywa na Wakristo hatua kwa hatua katika maisha yao ya kila siku. Kwa sasa Baba Mtakatifu anajiandaa kushiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya mageuzi ya Kiluteri duniani. Kumbe, Baba Mtakatifu Francisko atashirikiana na viongozi wengine wa Makanisa katika maadhimisho haya kuanzia tarehe 31 hadi 1 Novemba 2016, huko nchini Uswiss.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.