2016-10-12 09:35:00

Mwongozo wa maisha ya Kikristo!


Katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho, mwamini anakutana na upendo wenye huruma unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kuweza kuzima kiu ya amani ya ndani inayodhihirishwa na kila mwamini. Hivi ndivyo anavyoandika Baba Mtakatifu Francisko katika utangulizi wa kitabu cha “Mwongozo wa maisha ya Kikristo”  kinachozungumzia kwa kina na mapana kuhusu “Dhambi, Huruma ya Mungu, Upatanisho. Kamusi ya Kitaalimungu na Shughuli za Kichungaji”. Kitabu hiki kimehaririwa na Idara ya Uchapaji ya Vatican.

Kitabu hiki ambacho ni msaada mkubwa kwa Wakleri na waamini katika ujumla wao, kimezinduliwa rasmi, tarehe 11 Oktoba 2016 na Kardinali Velasio de Paolis aliyepembua kwa kina na mapana hatua kuu ambazo historia ya mwanadamu imepitia, yaani: Uumbaji, dhambi, ukombozi unaojikita katika huruma ya Mungu na msamaha wa dhambi pamoja na upatanisho. Katika safari hii ya maisha, mwanadamu anajitambua kuwa ni mdhambi na anayeinua uso wake kwa Baba mwenye huruma, ili kuomba huruma na msamaha wa dhambi zake.

Kardinali De Paolis anakaza kusema, Baba mwenye huruma na mwingi wa upendo usiokuwa na kifani anamkirimia mwanadamu msamaha unaomwezesha mwamini kuonja mabadiliko ya ndani katika maisha yake, tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa urafiki na Mwenyezi Mungu ambaye amemponya na madonda yake ya dhambi pamoja na kumkirimia neema ya kudumu katika ujenzi wa urafiki na Mwenyezi Mungu. Kamusi hii ni msaada mkubwa kwa waamini hasa wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kipindi cha toba na wongofu wa ndani unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Kamusi hii inalenga kuwa ni mwongozo wa jumla wa safari ya maisha ya Mkristo anasema Kardinali Mauro Piacenza, Kiongozi mkuu wa Toba ya Kitume wakati alipokua anaoa utambulisho wa jumla kwa ajili ya mchakato wa uzinduzi wa Kamusi hii. Ni kitabu ambacho kinaweza kuwa na mafao makubwa kwa Jumuiya za waamini, watawa na mwamini mmoja mmoja anayetaka kujitajirisha kwa kujizamisha katika bahari ya huruma ya Mungu, ili kumwambata Kristo aweze kuwa ni Bwana na Mwalimu wake wa maisha, tayari kumshuhudia katika maisha adili na matakatifu.

Kamusi hii ina utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho unaobubujika kutoka katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, lakini zaidi kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, inayomwonjesha mwamini huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake! Wahusika wakuu pia walipata nafasi ya kushirikisha utajiri wa Kamusi hii katika maisha na utume wa Kanisa, ili waamini waendelee kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.