2016-10-12 14:36:00

Mji wa Dodoma unapaswa kupangwa vyema ili ulete mvuto!


Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameikaribisha kampuni ya ujenzi ya Moladi Tanzania ielekeze nguvu zake Dodoma ambako kuna mahitaji makubwa ya nyumba za watumishi. “Natambua kuwa mnatumia teknolojia ya kisasa na ujenzi wa nyumba zenu unachukua siku chache sana. Ninawaencourage mje Dodoma ambako kuanzia Machi mwakani, watumishi wengi wataanza kuhamia huko,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa wito huo Jumatano, Oktoba 12, 2016 wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Abeid Abdallah ambaye alifika ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam na kumuonyesha ramani ya nyumba za watumishi ambazo wanazitumia. Waziri Mkuu amesema Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ina maeneo ambayo imeyatenga rasmi kwa ajili ya viwanja vya makazi na anaamini katika muda wa miezi miwili wanaweza kujenga nyumba za kutosha watumishi wanaotarajiwa kuhamia katika awamu ya pili.

“Nimeangalia michoro yenu, nyumba za vyumba vitatu vya kulala zina hadhi ya kukaa hata wakurugenzi; na watumishi wa kawaida wanaweza kumudu zile za vyumba viwili vya kulala… ninawatia moyo mwende haraka Dodoma na wale ambao wako serious wataleta maombi yao mara moja,” amesema. Waziri Mkuu amesema amefarijika kuona kuwa size ya ramani zao inatosha kwenye kiwanja cha ukubwa wa mita za mraba 550 ambacho ni high density na watumishi wengi wanaweza kumudu kuvinunua.

Kwa upande wake, Mkurugenzi huyo, Bw. Abdalla amemweleza Waziri Mkuu kwamba nyumba ya ukubwa wa vyumba vitatu vya kulala, yenye sebule, jiko, stoo na choo inatosha eneo la mita za mraba 94 tu.  “Kati ya vyumba hivyo vitatu, kimoja ni master, pia kuna sebule, chumba cha kulia na kibaraza. Hii inaanzia shilingi milioni 35 hadi milioni 41 kutegemea na aina ya vifaa unavyoweka kwenye umaliziaji. Lakini tukiongeza na servant quarter utalazimika kulipia shilingi milioni 7 ambapo unapata vyumba viwili na choo na bafu ndani,”amesema.

“Kimsingi, ni lazima tutaweka madirisha, milango, vyoo, masinki ya bafuni na jikoni, tiles (na mtu anaruhusiwa kuchagua za China, Italy au Spain),”ameongeza. Akifafanua kuhusu nyumba yenye vyumba viwili vya kulala, Bw. Abdalla amesema nayo pia ina sebule, jiko, stoo na choo kimoja na inatosha eneo la mita za mraba 54. Amesema nyumba hizo zinaanzia sh. milioni 20 hadi 25 kutegemeana na aina ya vifaa vinavyowekwa kwenye umaliziaji. Amesema ujenzi wa nyumba moja unachukua wiki sita na kama viwanja viko eneo moja au jirani, wanaokoa muda wa siku tatu hadi tano kwa kila nyumba. “Tunajenga ukuta kwa kumwaga theluji isiyochanganywa na kokoto ambayo ni mchanganyiko wa saruji, mchanga na kemikali. Inakauka baada ya saa saba na ukuta wetu ni imara mara nne zaidi ya ukuta uliojengwa na tofali la zege.”

Teknolojia yetu inawezesha ukuta wa nyumba nzima kukamilika ndani ya siku sita, nyumba zetu zinastahimili matetemeko, vimbunga na ujenzi wake unapunguza gharama za ujenzi kwa asilimia 40. Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa nyumba hizo, Bw. Abdalla amesema wana mikataba na mabenki kwa hiyo wanaweza kujenga nyumba na kuziuza mara moja lakini pia wananchi wanaweza kuingia mikataba na mabenki na kulipia kidogo kidogo katika muda maalum (mortgage).

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mji wa Dodoma ni lazima upangwe ili uwe tofauti na miji mingine hapa nchini. Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumatano, Oktoba 12, 2016 wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Abeid Abdallah ambaye alifika ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam na kuelezea nia yake ya kutaka kuwekeza mjini Dodoma. Amesema Serikali haitaki kurudia makosa yaliyofanyika kwenye miji mingine. “Katika kuupanga ule mji, ni lazima mji upangwe kama ambavyo miji mingine mikuu inapangwa. Kila eneo kutakuwa na nyumba za aina fulani. Hatuwezi kuachia watu wajenge popote na wanavyotaka, mji unakuwa haupangiki. Na hilo ndilo kosa lililofanyika kwenye miji mingine mikubwa ambayo tunayo kwa sasa.”

Amesema Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya kuhamia Dodoma imepewa jukumu la kupitia upya Master Plan ya mji wa Dodoma na kuainisha maeneo ambako nyumba za aina mbalimbali zitajengwa. “Kimsingi tunataka tuanze kujenga miji iliyopangiliwa na Dodoma tunataka uwe wa mji kwanza kuujenga vizuri kwa standard ya sasa. Kutakuwa na nyumba za ghorofa katika maeneo fulani, na nyumba za kawaida katika maeneo fulani. Mkurugenzi wa CDA amekwishaandaa ramani rasmi,” amesema.

Akizungumzia kuhusu ujenzi kwenye maeneo ambayo tayari wananchi wanaishi, Waziri Mkuu amesema Serikali itaweka utaratibu ili kuwe na mikataba baina ya mwekezaji na mwananchi anayemiliki eneo husika ili asinyimwe haki ya kumiliki eneo lake. “Kama tutahitaji eneo ambalo tayari lina makazi, taratibu zetu ni zilezile kwamba tutaweka mikataba kati ya mwekezaji na mwananchi. Kama anataka kujenga kwenye eneo lile, basi lazima amhusishe mwenye eneo na kama anataka kujenga ghorofa ni lazima ahakikishe mwenye eneo anapata umiliki kama tulivyofanya kule Magomeni,”amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi huyo, Bw. Abdalla amemweleza Waziri Mkuu kwamba wako tayari kushirikiana na Serikali katika zoezi la Serikali kuhamia Dodoma kwa lengo wa kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini kupata makazi bora na ya kudumu.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.








All the contents on this site are copyrighted ©.