2016-10-11 10:10:00

Ni kwa heshima ya wananchi wa Syria wanaoteseka sana!


Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Askofu mkuu Mario Zenari kuwa ni kati ya Makardinali wapya watakaosimikwa rasmi kwenye mkutano wa Makardinali utakaofanyika hapo tarehe 19 Novemba 2016 katika mkesha wa kufunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu amekaza kusema, Kardinali mteule Zenari ataendelea na utume wake kama Balozi wa Vatican nchini Syria, ambako mtutu wa bunduki bado unaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Kardinali mteule Zenari katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, amepokea taarifa za uteuzi wake kuwa Kardinali kwa mshangao mkubwa na kwamba, anapenda kumshukuru Baba Mtatakatifu Francisko, kwani dhamana hii ni kwa ajili ya heshima na kumbu kumbu endelevu ya mateso na mahangaiko ya wananchi wa Syria ambao kwa muda wa miaka mitano wamekuwa wakiishi katika hali ya wasi wasi na mashaka kutokana na vita. Kardinali mteule anasema, anapenda kutolea heshima hii kwa wale wote waliopoteza maisha na wanaoteseka kutoka na vita nchini Syria.

Uwepo endelevu wa Kardinali mteule Zenari ni ushuhuda tosha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufanya hija na wananchi wa Syria katika shida na mahangaiko yao, licha ya Jumuiya ya Kimataifa kushindwa hadi sasa kupata suluhu ya kudumu juu ya mgogoro wa vita unaoendelea nchini humo. Hii ni mara ya kwanza katika historia kwamba, Askofu mkuu anateuliwa kuwa Kardinali na kuendelea kutekeleza utume wake kama mwakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kwa unyenyekevu mkubwa anasema Kardinali mteule Zenari kwamba, uteuzi wake kushika wadhifa huo si mali kitu kutokana na vita inayoendelea nchini Syria, lakini ni alama wazi kwamba, Kanisa liko bega kwa bega na familia ya Mungu nchini Syria licha ya magumu na changamoto inazokumbana nazo. Kardinali mteule Zenari anatambua kuwa Baba Mtakatifu Francisko yuko nyuma yake, anaunga mkono juhudi za upatikanaji wa haki, amani, usalama, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kardinali mteule Mario Zenari mwenye umri wa miaka 70 ana uzoefu wa miaka 36 katika huduma ya kidiplomasia hasa katika maeneo tete na yenye vita. Tangu mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Syria. Hii ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: amani, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi badala ya mataifa yenye nguvu kusimamia masilahi yake binafsi. Hapa Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutambua kwamba, wanaoteseka zaidi kutokana na vita hii ni watoto, wanawake na wazee, watu ambao hawana hatia. Kuna uvunjifu mkubwa kwa haki msingi za binadamu na kwamba, matumaini na hatima ya wananchi wa Syria iko mikononi mwa Jumuiya ya Kimataifa, ambayo kimsingi hadi sasa imegawanyika kutokana na kinzani za kimasilahi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi pia kuhakikisha kwamba, misaada ya kiutu inawafikia walengwa, ambao kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na vita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.