2016-10-11 13:51:00

Mchakato wa mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu nchini Mali


Serikali ya Ujerumani inasema, itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mali katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na dawa za kulevya, mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu; haki, amani na utulivu. Hayo yamesemwa mapema Juma hili na Chancellor Angela Merkel alipokutana na Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali. Bi Angela Merkel kwa sasa anatembelea Niger na Ethiopia.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema kwamba, hali bado ni tete sana nchini Mali licha ya mkataba wa amani uliotiwa mkwaju kunako mwaka 2015 kati ya Serikali na Kikundi cha waasi cha Tuareg pamoja makundi yenye silaha, yaliyokuwa yanatishia amani na utulivu nchini Mali. Ujerumani itaendelea kusaidia mchakato wa ushirikiano na maendeleo kwa ajili ya mali katika maboresho ya huduma ya afya, maji safi na salama sanjari na kudhibiti wimbi kubwa la wahamiaji kutoka Mali linalotaka kukimbilia Ulaya ili kutafuta maisha bora zaidi.

Serikali ya Ujerumani inakaza kusema, kamwe Serikali ya Mali isikubali Bahari ya Mediterrania kugeukwa kuwa ni kaburi la wahamiaji haramu wanaotafuta fursa za maisha bora Barani Ulaya kwa kuweka rehani maisha yao. Kimsingi, wahamiaji wengi wanakufa kwa kiu na utupu wanapojaribu kuvuka Jangwa la Sahara, lakini wengi wao wanakufa maji kwenye Bahari ya Mediterrania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.