2016-10-11 08:15:00

Kenya simameni kidete kufanikisha uchaguzi mkuu 2017!


Haki, amani, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha utulivu na demokrasia ya kweli! Haya ni mambo msingi ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na familia ya Mungu nchini Kenya, wakati huu inapojiandaa kwa ajili ya mchakato wa uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika nchini humo, mwezi Agosti, 2017.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Peter Kairo wa Jimbo kuu la Nyeri, Kenya, wakati wa Ibada ya kuombea taifa la Kenya iliyofanyika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria ya Subukia, huko Nakuru. Askofu mkuu Kairo, amewataka wananchi wa Kenya kutorudia tena makossa yaliyojitokeza kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika kati ya mwaka 2007/2008 ambao ulipelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao, kiasi hata cha kuliacha taifa likiwa limemeguka katika dhana ya ukabila, udini na ubinafsi!

Askofu mkuu Kairo amewataka viongozi wa kisiasa wanaowania nafasi mbali mbali za uongozi pamoja na wapambe wao, kuacha mara moja tabia ya kuwagawa wananchi wa Kenya kwa misingi ya ukabila na udini, kwani ni mambo ambayo hayana tija wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Kenya. Ameyataka Majimbo Katoliki nchini Kenya, kusaidia kuwaelimisha wananchi, ili hatimaye, waweze kuwajibika kikamilifu wakati wa mchakato mzima wa upigaji kura badala ya kuuza kura zao kwa “kipande cha Kitenge”.

Askofu mkuu Kairo katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma katika medani mbali mbali ya maisha. Wakristo wawe kweli ni chemchemi ya huruma ya Mungu kwa watu. Ibada hii ya Misa Takatifu ilihudhuriwa na idadi kubwa ya Maaskofu wa Majimbo Katoliki Kenya waliokuwa wameandamana na waamini kutoka katika Majimbo yao.

Na Rose Achiego!

Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.