2016-10-11 07:30:00

Jifunzeni fadhila ya unyenyekevu hata kutoka kwa "wanyamahanga"!


Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, Rozari takatifu ni muhtasari wa historia ya huruma ya Mungu kwa binadamu na kwamba, waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, ili aweze kuwaokoa na hatari zote za maisha ya kiroho na kimwili! Kwa ufupi huu ndio ujumbe uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa maadhimisho ya Jubilei ya Bikira Maria, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumamosi, tarehe 8 Oktoba 2016.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake kwenye kilele cha Jubilei ya Bikira Maria katika kipindi hiki cha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Jumapili tarehe 9 Oktoba 2016, amekazia kwa namna ya pekee fadhila ya unyenyekevu kutoka kwa Bikira Maria pamoja na kujifunza mema na mazuri kutoka kwa jirani, ambao wakati mwingine ni wageni au waamini wa dini nyingine. Hivi ndivyo ilivyomshangaza Yesu alipowaponya wakoma kumi waliokuwa wanatembea katika njia ya kifo, lakini kwa imani na matumaini yao, akawaonesha njia ya ufufuko kwa kuwagusa na kuwaponya mahangaiko yao. Jambo la kushangaza ni kuona kwamba, kati ya wale wakoma kumi ni mmoja tu aliyerejea kwa Yesu kumtolea Mungu sifa na shukrani kwa kumponya.

Huyu ni Msamaria, ambaye kwa wengi alijulikana kuwa ni “Mtu wa kuja” “Kyasaka” “Mnyamahanga” na “Mpagani” ndiye pekee aliyethubutu kushuhudia kilele cha imani yake kwa kumtolea Mungu sifa na shukrani kwa njia ya Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwanadamu! Ni Mungu aliyeweza kumsimamisha tena na kumwokoa, kiasi hata cha kumkirimia nafasi ya kumkaribisha na kutembea kati ya wanafunzi wa Yesu. Mpagani huyu ni ushuhuda makini wenye mvuto katika kushukuru, kusifu na kumtukuza Mungu. Hapa waamini wajenge utamaduni wa kushukuru!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake anakaza kusema, katika maadhimisho ya Jubilei ya Bikira Maria, Kanisa linamweka Bikira Maria mbele ya waamini, aliyebahatika kupokea ujumbe wa Habari Njema ya kuzaliwa kwa Masiha Yesu, akaonesha moyo wa shukrani kwa utenzi wake maarufu kama “Magnificat”. Ni Mama alitambua zawadi ya Mungu katika maisha yake, akaonesha shukrani na kushuhudia furaha ya Injili ikibubujika moyoni mwake.

Huu ndio unyenyekevu ulioneshwa pia na Naaman mtu wa Mungu aliyeponywa ukoma akakubali kupokea changamoto kutoka kwa Nabii Elisha na kwenda kujichovya mara saba kwenye Mto Yordani na ngozi yake ikawa kama ya mtoto mchanga. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Moyo Safi wa Bikira Maria ni kielelezo madhubuti cha unyenyekevu, kiasi hata cha kuwa tayari kupokea zawadi ya Mungu, kiasi hata cha Mwenyezi Mungu kuamua kufanya makazi tumboni mwa Bikira Maria na hapo akawa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu awakirimie fadhila ya unyenyekevu badala ya kujificha katika usalama wa mali na utajiri, akili pamoja na mafanikio binafsi. Waamini wajifunze kuwaheshimu na kuwathamini na kujifunza kutoka kwa majirani zao, hata kama ni waamini wa dini nyingine. Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ilionja pia machungu ya kuishi uhamishoni, lakini imani yake, iliiwezesha kushinda magumu na vishawishi ilivyokumbana navyo katika maisha! Bikira Maria alibahatika kuwa kweli ni mama wa shoka katika imani, shukrani na mapendo! Daima yuko mbele ya Yesu, ili kumshukuru kwa huruma na upendo anaowakirimia waja wake!

 

Mara baada ya misa takatifu, Papa alitumia muda mrefu kuzungumza na kusalimiana na Wakleri, baadaye akapanda kwenye gari la wazi, ili kusalimiana na bahari ya waamini waliokuwa wamehudhuria maadhimisho ya Jubilei ya Bikira Maria kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.