2016-10-10 11:33:00

Ogopa ukoma unaopekenyua maisha ya kiroho!


Moja ya kauli za hekima alizowahi kuzitamka Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa uhai wake ni ile inayolinganisha dhambi ya ufisadi au ya rushwa na ugonjwa wa ukoma aliposema: "Mkimuona mtu anaitafuta Ikulu kwa pesa muogopeni kama Ukoma. Mimi nimekaa Ikulu miaka 25, ikulu sio mahali pa kukimbilia." Jinsi ugonjwa wa ukoma unavyotisha, unavyoharibu viungo vya binadamu na kumfanya mgonjwa atengwe na jamii ndivyo ilivyo kwa fisadi na mla rushwa.

Hapo zamani ukoma ulikuwa ni ugonjwa wa hatari na wa kutisha sana. Kwa Kiebrania ukoma unaitwa Sarakhathe, kutokana na neno-tendo Sara lenye maana ya kuadhibiwa au kulaaniwa na Mungu. Hiyo ilikuwa ni adhabu au kiboko cha Mungu kutokana na kufuru alizofanya binadamu dhidi ya Mungu na binadamu, kama vile kumkana Mungu, kuua, uzinzi, ufisadi, rushwa, udanganifu, ujangili, nk. Mgonjwa wa ukoma alifananishwa na mfu anayetembea. Kupona kwa ukoma kulikuwa ni kama kufufuka toka wafu, kazi iliyoweza kuifanya Mungu peke yake. Ndiyo maana mfalme Yoramu wa Israeli alitishika sana alipopata barua kutoka kwa mfalme Benadadi wa Shamu (Siria) iliyomwomba kumponya ukoma mwanajeshi na waziri wake mkuu Naamani.

Mfalme wa Shamu aliandika barua iliyosema: “Waraka huu utakapokuwasilia, tazama, nimemtuma mtumishi wangu Naamani kwako, ili upate kumponya ukoma wake.” Yoramu alipoisoma barua hiyo akatambua mara moja kuwa anatafutiwa ubaya, akasema: “Je, mimi ni Mungu, niue na kuhuisha, hata mtu huyu akanipelekea mtu nimponye ukoma wake? Fahamuni, basi, nakusihini, mwone ya kuwa mtu huyu anataka kugombana nami.” (2Wafalme 5:1-7)

Jinsi ukoma unavyomharibu na kumchafua mtu viungo vyake vya mwili hadi kushindwa kutambulika, ndivyo dhambi inavyoweza kumchafua mtu hadi asitambulike kadhalika mdhalimu, mwonezi, mwizi, jambazi, mwuaji , mla rushwa, na fisadi anaharibika utu wake hadi kuchukiza na kutotambulika. Kadhalika, kama vile ukoma unavyoua vionjo vya mwili hadi mgonjwa hawezi kusikia maumivu., yaani, mkoma anaweza kukatika kiganja cha mkono asigundue wala kuonja maumivu. Kadhalika mdhambi hana vionjo vyovyote vile mbele ya thamani za maadili, na haonji kabisa juu ya kitu gani ni dhambi inayoweza kumdhuru.

Kutokana na hali yao ya kuharibiwa mwili na ya kunuka, waliepukwa na kutengwa na jamii hata na familia zao. Hivi wakoma wakaishi peke yao pamoja utengoni. Katika Agano la Kale walipewa sheria walizolazimika kuzishika, kama vile kuvaa malapulapu ili watambulike kila wanapopita, walitakiwa kuacha kichwa wazi, wafunike mdomo wa juu tuu na kupiga kelele ‘Ni najisi! Ni najisi!’ aidha “Siku zote ambazo pigo li ndani yake, yeye alikuwa najisi; alikaa peke yake, na makazi yake yalikuwa nje ya mrago.” (Walawi 13). Hali hiyo inatokea pia kwa mkoma wa kiroho, anatengwa na watu kwa sababu wanamwogopa, kama alivyosema mwalimu Nyerere, “waepukeni mafisadi na wala rushwa kama ugonjwa wa ukoma.”

Leo, Yesu anasafiri kutoka Galilea kwenda Yerusalemu akipitia Samaria. Njiani anakutana na wagonjwa kumi wa ukoma. Hebu tufuatilie kidogo mazingira wanakotoka wakoma hawa na idadi yao. Wakoma hawa wanatoka kijijini. “Alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kmi wenye ukoma.” Kadiri ya Agano jipya, Kijijini wanakaa wakazi wenye fikra moja waliobobea katika mila na utamaduni wao. Wanakijiji hao wanamfikiria mkoma kuwa ni mdhambi, mtu wa ovyo, mchafu, si mtu kamili, mtu wa kumkwepa kwani ametengwa na kulaaniwa na Mungu. Yesu anaingia huko kijijini na kwa Neno lake anaingiza mahusiano mapya na wagonjwa wa ukoma katika kijiji hicho.

Aidha idadi ya wakoma ni kumi, ikimaanisha ukamilifu. Namba hii inawajumlisha wanavijiji (wakazi) wa Kiyahudi na Wasamaria alimopita Yesu akitokea Galilea kwenda Yerusalemu. Hapa ikumbukwe pia kwamba Wayahudi na Wasamaria walibezana na kukaliana kiuadui. Wanakijiji hao wanapogundua kuwa wote ni wakoma (wachafu, wametengwa) wanaacha utofauti wao, wanashikamana na kwenda kumlilia Yesu kwa pamoja: “Yesu Mwalimu utuhurumie.” Kwa Kigiriki Iesou epistata  eleeson. Neno epistata au epistatesi limefasiriwa kuwaa ni “mwalimu” kumbe, lina maana ya “Yesu uliye mkuu” Huyu ndiye aliyeanzisha utawala mpya badala ya ule unaowatenga wachafu na wasafi; wadhambi na watakatifu. Wakoma hawa hawakutafuta kuponywa kila mmoja peke yake, bali kama jumuia na kutaka kukombolewa kama jumuia na siyo kama mtu  binafsi.

Kumbe, sisi sote ni watoto wa baba mmoja, sisi sote tu wakoma tunaishi katika kijiji kimoja (global village) na tunahitaji Neno litakalotuponya na kutufanya wote tuwe wazuri na kupendana. Tujifunze kutoka kwa wakoma hawa tabia ya kupokeana, ya kukubaliana kwa vile sisi sote tunao ukoma. Kwa pamoja tumwendee Yesu na kuomba kuponywa kama tunavyosali katika Misa kwa pamoja “Kyrie eleeison, Christe eleeison” yaani Bwana utuhurumie, Kristo utuhurumie. Yesu akawaambia: “Enendeni mkajioneshe kwa makuhani.” Wagonjwa hawa waliamini Neno la Yesu kuwa linaweza kuwaponya ukoma wao uliowafanya wachukiwe, wakose kusikia maumivu, na hata kutengwa, hapo wakaondoka na kwenda kujionesha kwa makuhani.

 

“Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika.” Yaani wakiwa safarini wanatembea kuelekea kwa makuhani baada ya kulisikia na kutegemezwa na Neno linalookoa na kuponya ukoma wao. Neno la nabii Eliseo ndilo lililomponya Namaani. Naye Naaman akalisadiki neno la Nabii Eliseo, akaenda kujitumbukiza kwenye mto Yordani na ngozi yake ikawa safi kama ya mtoto. Kwa yule anayeamini Neno la Bwana ataponywa na ukoma wake (dhambi zake) na ngozi ya mwili wake itageuka kuwa kama ya mtoto mchanga.

Maisha yetu ya kikristu, yanalinganishwa na safari. Uponyaji wa ukoma ni mfano wa uponyaji wa ndani upatikanao kwa kusikiliza na kulishika Neno la Yesu. Neno la Bwana (Injili) linatuongoza katika safari ya maisha yetu na linatuponya polepole kasoro na dosari tulizo nazo tunaposafiri hapa duniani kuelekea kwa Mungu. Kwa hiyo kwa njia ya Neno la Yesu tunaalikwa kutembea kwa uvumilivu, kwa subira, na kwa matumaini. “Na mmoja wao alipona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu; akaanguka kifudifudi miguu pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria.” Yesu akaangalia na kusema: “Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?”.

Yesu anashangaa kumwona mtu mmoja tu anarudi kumpa Mungu utukufu. Masikitiko ya Yesu hayakuhusu kupewa shukrani la hasha. Angalia alichofanya yule Msamaria: “Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu.” Kadhalika na maneno ya Yesu: “Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu?” Kwanza aliyerudi ni mgeni na siyo Myahudi. Mgeni ni yule msamaria hakuwa ameelimishwa Torati na hakujua matendo ya Masiha. Kumbe, Myahudi alikuwa ameelimishwa Agano la kale na Torati. Walikuwa walielimishwa na kutayarishwa kwa muda mrefu kulipokea Neno la Masiha linaloponya kila aina ya ukoma.

Pili, “Kumpa Mungu utukufu au kumshukuru maana yake, ni kukiri, kutambua na kufaidi matendo ya ukombozi aliyoufanyia Mungu ulimwengu na kumpa utukufu anaostahili. Sababu za kumpa Mungu utukufu tunazikuta katika Zaburi 136, hasa kutokana na maajabu aliyoyafanya: “Mshukuru Bwana kwa kuwa ni mwema, kw maana fadhili zake ni za milele. Yeye peke yake afanya maajabu makuu, kwa maana fadhili zake ni za milele. Alivyokomboa Waisraeli, amewapa chakula woe, kwa maana utukufu wake ni wa milele.”

Maajabu ya Mungu ni mengi na makubwa aliyotutendea binadamu: Ametupa jua, mwezi, hali nzuri ya hewa, mvua, mito na ardhi hadi tunaweza kulima na kupata chakula, kuna misitu, wanyama nk. Kwa hiyo kupa Mungu utukufu maana yake kufaidi maisha na kujua kwamba maisha hayo yanatoka kwa Mungu na yana malengo. Msamaria alimpa Mungu utukufu kwa kuwa alitambua kuwa Neno la ukombozi lilitoka kwa Mungu. Mshangao wa Yesu ulikuwa ni ule wa kuona Wayahudi waliokuwa wameandaliwa kumbe hawakuwa wamefikia mara moja kutambua ukombozi wa ukoma wetu unatoka wapi. Walishindwa kabisa kuelewa kwamba ukombozi unapatikana kutoka katika Neno la Bwana.

Yesu anamwambia huyu Msamaria “Inuka enenda zako, imani yako imekuokoa.” Kuokoka maana yake, ni kujiacha kuwa huru na ukoma wetu, kwa kupokea Neno la ukombozi linalotoka mdomoni mwa Yesu. Pale unapopokea na kuaminia neno hilo unakuwa mtu mwema mzuri siyo aliyetengwa, bali mwenye kulingana na upendo wa Mungu. Imani kwa Yesu ndiyo inayotenda muujiza huo. Neno hilo hutenda kazi kwakati tunasafiri katika maisha. Huo ndiyo ujumbe wa kituko cha leo, kwamba katika safari ya maisha haya tushikamane, tujisikie kuwa sisi sote ni ndugu, sisi sote tu wakoma yaani tuna dhambi. Tutambue kwamba katika safari ya maisha tunaongozwa na Neno la Injili linatufana kuwa sawa, na Neno hilo la uponyaji linalotoka kwake.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.