2016-10-10 08:59:00

Kanisa nchini Colombia kuendelea kuchangia mchakato wa amani!


Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia limepokea kwa moyo wa imani, matumaini na shukrani tuzo ya amani aliyopewa Rais Juan Manuel Santos kwa kutambua mchango wake katika mchakato wa ujenzi wa amani, mshikamano na umoja wa kitaifa nchini humo. Akizungumzia kuhusu tuzo hii, Askofu mkuu Rubèn Salazar Gòmez wa Jimbo kuu la Bogotà, Colombia ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu katoliki Amerika ya Kusini, CELAM anasema, hii ni hatua muhimu sana, ingawa Kanisa linaonesha wasi wasi kutokana na wananchi kutokubaliana na mchakato wa amani nchini humo kwenye kura ya maoni iliyopigwa nchini humo hivi karibuni!

Jumuiya ya Kimataifa inaonesha matumaini makubwa kwa Colombia kuweza kufikia ufumbuzi wa amani baada ya mgogoro wa vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa takribani miaka hamsini na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kanisa nchini Colombia linapenda kushiriki kikamilifu katika utekelezaji na uimarishaji wa mkataba wa amani nchini humo, tukio ambalo linaweza kupambwa kwa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia kwa mwaka 2017.

Watu wenye mapenzi mema wanataka kuona amani, upendo na mshikamano vinatawala nchini Colombia ili kuondokana na utamaduni wa kifo ambao umesababisha chuki, uhasama na utengano kati ya watu. Licha ya kura ya maoni kupinga mchakato wa Serikali ya Colombia kufanya majadiliano na Kikundi cha waasi wa FARC, bado kuna umati mkubwa wa wananchi wa Colombia una matumaini ya kuweza kupatikana kwa amani na utulivu nchini mwao.

Askofu mkuu Gòmez anasema, changamoto kubwa hapa ni haki, ili kweli amani, upatanisho na umoja wa kitaifa viweze kushika mkondo wake. Kuna maelfu ya watu waliouwawa na wengine wengi kutekwa nyara na kufanyishwa vitendo vya kinyama na kikundi cha waasi wa FARC, matukio ambayo bado yameacha kurasa chungu katika maisha ya wananchi wengi wa Colombia. Serikali nayo kwa upande mwingine inatuhumiwa kwa kutenda kinyume dhidi ya ubinadamu. Je, wahusika wa vitendo hivi wanaweza kuhukumiwa namna gani na bado mkataba wa amani ukaendelea kushika mkondo wake?

Bado wananchi wengi wa Colombia wana wasi wasi kuhsu ushiriki wa kiongozi wa waasi katika masuala ya kisiasa nchini humo na kuanza kushiriki katika mchakato mzima wa demokrasia. Changamoto zote hizi zinalifanya Kanisa nchini Colombia kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, mchakato wa haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa vinaimarishwa na kudumishwa; mambo msingi yatakayosaidia kuharakisha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia kwa mwaka 2017.

Mkataba wa amani kati ya serikali na kikundi cha waasi kimsingi ni suala la kisiasa, lakini ikumbukwe kwamba, amani inapaswa kujengeka kutoka katika akili na nyoyo za watu kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani; msamaha na upatanisho wa kweli. Katika mwelekeo kama huu, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko inakuwa ni zawadi kubwa katika kuimarisha mchakato wa amani ya kweli nchini Colombia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.