2016-10-04 15:15:00

Papa awatembelea waathirika wa tetemeko la ardhi Amatrice


 

Mapema Jumanne, 04 Oktoba 2016, Baba Mtakatifu Francisko amefanya ziara ya kushtukiza katika maeneo yaliyokumbwa vibaya na tetemeko la aridhi ,  lililotokea katika eneo la kati nchini  Italia ,  tarehe 24Agosti 2016. Papa amefanya ziara hii kama tendo la huruma, kwenda kukutana, kuwafariji na kuonyesha mshikamano wake kwa waathirika,  na hasa waliopoteza ndugu zao na makazi yao kutokana na uharibifu mkubwa wa majengo hasa katika mji wa  Amatrice.  Akiwa katika eneo hilo, Papa Francisko aliitembelea shule ya msingi ya muda iliyoanzishwa katika eneo hilo kwa msaada wa kikosi cha usalama wa raia cha Trento , na kisha akaenda karibu na eneo lililoharibiwa vibaya zaidi, kujionea mwenyewe uhalibifu uliofanywa na jenga hili, sehemu ambayo kwa sasa haruhusiwi mtu yeyote kuishi. Na pia alipita katika eneo la  Arquata del Tronto, Accumoli.

Katika eneo la shule  ya msingi aliandamana na  Askofu wa Rieti,  Askofu  Domenico Pompili,  na  alikutana na wanafunzi na walimu, na watoto wanafunzi bila kuchelea walimtumbuiza kwa nyimbo za kirafiki na kumpatia zawadi ya michoro yao ya kitoto,  inayowakumbusha uwepo wa janga hili. Na kisha alitoa hotuba yake fupi,  kwa watu waliokuwa wamemzunguka, ambamo aliwahakikishia ukaribu wake na kuwaomba pia wasimsahau katika sala zao.

Papa Francisko mara baada ya kupata taarifa za janga hili la tarehe 24 Agosti, Jumapili iliyofuatia wakati wa sala ya Malaika wa Bwana tarehe 28 Agosti , ikiwa imepita siku nne baada ya tetemeko, alionyesha hamu yake ya kutaka kwenda kukutana na waathirika wa tetemeko , kama tendo la huruma. Kukutana na kuwapa maneno ya kuwafariji  katika tumaini la Kikristo .

Na Jumapili iliyopita, wakati wa mkutano wa waandishi akirejea kutoka  mjini Baku kwa  ndege, Papa Francisko alisema, alirudia kuonyesha hamu yake ya  kufanya  ziara katika mazingira ya  faragha,  kuwatembelea wahanga wa tetemeko la aridhi katika mjiwa wa Amatrice,  kama Padre, kama askofu na , kama Papa, bila msafara rasmi. Alipenda kuwa karibu na watu  hao, hamu aliyoitimiza Jumanne hii.








All the contents on this site are copyrighted ©.