2016-09-27 08:50:00

Rais Joseph Kabila wa DRC atembelea Vatican


Jumatatu 26 Septemba,  Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)Joseph Kabila Kabange, alitembela Vatican na kukutana na Papa Francisko na kisha  alikutana na Askofu Mkuu Paulo Gallagher , Katibu wa Vatican kwa ajili ya mahusiano na nchi zingine.

Mazungumzo yao yalifanyika katika hali ya kirafiki, yakionyesha  uhusiano mzuri uliopo kati ya Jimbo Takatifu na DRC. Kwa namna ya kipekee walitazama uhusiano wa  Kanisa Katoliki katika maisha ya kijamii , kupitia  kazi  zinazofanywa na taasisi za Kanisa, kumwendeleza mwananchi kielimu, kiafya  na kiuchumi hasa juhudi za kufukuza umaskini miongoni mwa jamii ya Congo.  Pande zote mbili zilionyesha kuridhika na makubaliano yaliyotiwa sahihi Mei 2016, kati ya Jimbo Takatifu na DRC.

Aidha jimbo la Papa bila kuchelea , lilirejea  kwa umakini zaidi hali ya kisiasa inavyosuasua katika taifa hilo, kama ilivyokuwa katika  machafuko ya hivi karibuni katika mji mkuu wa Kinshasa. Kwa upande huo , Jimbo la Papa limehimiza umuhimu wa serikali kujenga ushirikiano  thabiti  na  watendaji wengine wakuu wa kisiasa na wawakilishi wa vyama vya kiraia na jumuiya za kidini, kwa ajili ya ustawishaji wa mazuri kwa jamii nzima ya DRC,  kupitia njia ya  kuheshimu majadiliano na makubaliano yanayofikiwa kwa ajili ya  uwepo wa utulivu na amani ya  taifa.

Mwisho walizama zaidi  hali ya machafuko inavyotendea eneo la Kaskazini Mashariki mwa DRC, na kuona haja ya  ushirikiano zaidi  kitaifa na kimataifa kwa ajili ya utoaji wa msaada unaohitaji kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo.  








All the contents on this site are copyrighted ©.