Baba Mtakatifu Francisko Mapema Jumane hii akiongoza Ibada ya Misa katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta ndani ya Vatican, alizungumzia juu ya huzuni au mateso ya kiroho kutokana na misukosuko ya maisha kama maradhi na majanga. Alihoji nini hasa kinachotokea moyoni wakati tunapokumbwa na fadhaa ya kiroho? Homilia ya Papa ilitafakari kwa kina somo kutoka kitabu cha Ayubu, na kusistiza umuhimu wa maombi na sala ili kuyashinda yanayotia giza rohoni. Katika Ibada hii, pia Papa alifanya rejea katika historia ya maisha ya Mtakatifu Vincent de Paul , na pia aliwakumbuka Masista wa Mtakatifu Vincent , Mabinti wa Upendo , wanaofanya utume wao katika Jengo la Mtakatifu Marta la ndani ya Vatican, anakoishi Papa Francisko.
Mafundisho ya Papa Francisko , yaliutazama kwa kina wakati huu wa shida na mateso, kama ilivyokuwa kwa Ayubu , ambaye alipoteza kila kitu chake , si mali tu lakini pia watoto , hali iliyomletea kupoteza imani na kujiona kama amelaaniwa na Bwana. Papa alilinganisha wakati huu mgumu kwa Ayubu, na uzoefu wa maisha yetu , ambamo katika vipindi fulani pia tunakabiliwa na hali hiyohiyo ngumu na kukatiksha tamaa , ambamo tunaona kama hatuwezi tena kusonga mbele na maisha, ambamo roho husongwa na mfadhaiko mkubwa mbele ya uso wa Mungu, na kuwa sawa na mtoto mdogo aliyepoteza matumaini mbele ya baba yake. Kama pia ilivyokuwa pia kwa Nabii Yeremia, alivyomkasilikia Mungu.
Papa ameutafakari udhaifu huu wa kiroho alisema kwamba hutokea kwa kila mmoja wetu, katika hali mbalimbali wengine kwa nguvu zaidi na wengine katika kishindo cha kawaida, lakini kwa vyovyote vile, huleta giza moyoni , moyo kutaka tamaa , kutoona tena faida ya kuishi , kutamanai kufika mwisho wa safari ya maisha kwa hasira nyingi na mawazo mengi na kwa huzuni kubwa. Hali kama hizi Papa Francisko amesema , huidhoofisha roho na kupata hisia za kuangamia, kama vile hakuna tena maana ya kuishi ,mtu akiona heri kufa kuliko kuishi , kama kilivyokuwa kilio cha Ayubu.
Papa alieleza na kuhoji kumbe basi tufanye nini wakati tunapokutana na changamoto kama hizi , tunapopambana na hali ya kutia giza moyo , kupitia matukio mbalimbali katika maisha , kwa mfano majanga kwa familia, au magonjwa, jambo jingine lolote linaloshusha imani yetu? Jambo linalotukaba kiasi cha kukosa usingizi ? je tumezevidoge na kujimaliza au tubobee katika ulevi wa pombe au madawa ya kuelvya ? hivyo vyote havitasaidia kitu.
Papa ameshauri jawabu pekee kama ilivyo katika liturujia ya Neno la Mungu kwa siku hii, ni kuzama zaidi katika maombi na sala kwa Mwenyezi Mungu. Tunahitaji kuomba, kila wakati usiku na mchana ni kumlilia Mungu kwa nguvu kama alivyofanya Ayubu: mchana na usiku, ni kutoa kilio hadi sikio la Mungu lisikie.
Dawa pekee amesisitiza Papa, ni maombi. Kugonga kwa nguvu katika mlango wa Bwana na kummiminia matatizo yote , kumwambia, 'Bwana, Bwana , nisaidie naangamia. Maisha yangu yanaelekea kuzimu. Papa aliongeza, ni lazima tunapokuwa katika hali ya giza giza la kiroho, kuomba zaidi na zaidi na Bwana kwa haki atatenda kulingana na mapenzi yake.
Baba Mtakatifu Francisko ameeleza na kukamilisha kwa kumwomba Bwana, atupatie neema tatu: neema ya kutambua udhaifu wetu , neema ya kuomba tunapokabiliwa na changamoto na neema ya kujua watu wa kuongozana nao wakati wa mateso au nyakati mbaya za huzuni na mfadhaiko wa kiroho.
All the contents on this site are copyrighted ©. |