2016-08-24 08:48:00

Papa :Maisha si mchezo wa kuigiza bali ni utendaji halisi


(Vatican Radio) Baba Mtakatifu Francisko Jumapili katika hotuba yake fupi , kabla ya sala ya malaika wa Bwana,  alisema  kuwa maisha si mchezo wa video au maonyesha ya kuigiza, lakini ni utendaji  halisi ambao lengo lake  muhimu ni kufikia  wokovu wa milele.  Hayo aliyasema wakati akiwahutubia mahujaji na wageni waliokuwa wamekusanyika katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.  Maoni ya Papa yalilenga katika  mada ya wokovu wa milele, kama ilivyoelezwa katika Somo kutoka Injili ya Luka , ambamo Yesu akiwa njiani kuelekea Jerusalem , mtu mmoja alimwendea na kumwuliza iwapo wokovu ni kwa ajili ya watu wachache tu ( Luka 13:23).

Baba Mtakatifu akitafakri jibu la Yesu alisema  haijalishi wagapi wataokolewa  lakini cha muhimu ni mtu mwenyewe kujali wokovu wake. Na mlango wa wokovu upo katika kumfuata Yesu. Na tunaweza kuvuka kizingiti na kuingia maisha ya uwingu kwa huruma zake Mungu , na kwa njia ya upendo, na kwa kukishinda kiburi cha dhambi.  

Baba Mtakatifu aliendelea kufafanua kwamba ,katika  aya zilizosomwa,   Yesu  hakutoa jibu la moja kwa moja lakini alitoa jibu lake kwa namna nyingine ya mjadala ambayo , mwanzo mitume wake pia hawakuelewa  alipowaambia wajitahidi kuingia kwa kupitia mlango mwembamba; kwa  kuwa wengi,  watajaribu kuingia, lakini wao hawatafanikiwa (v.24).  Kwa  mfano wa Mlango, Papa aliendelea kufafanua kuwa  Yesu alipenda kuwaambia waliokuwa wakimsikilza  kwamba si suala la idadi ya watu watakaookolewa lakini la muhimu ni kila mtu ajue  njia  sahihi inayoongoza katika wokovu.

Na kuingia katika njia hiyo ni lazima mtu kupita katika mlango wake ambaye ni Yesu mwenyewe.  Yesu alisema 'Mimi ni mlango' kama ilivyoandikwa kaika Injili ya Yohana. Kumbe Yesu anatuongoza katika njia kwa usharika na Baba yake, ambamo tunaona upendo, maelewano na ulinzi. Lakini kwa nini mlango huu nyembamba? Papa pia alihoji na kueleza , Yesu alisema mlango mwembamba , si katika maana ya kukandamiza, au kuzia kupita, la hasha  lakini ni mwembamba kwa sababu, unataka mtu kuwa makini katika utendaji wake, si kuishi bila kuzingatia sheria za Mungu, bali  mlango huu ni kama kichujio, cha kuyaacha mabaya  na dhambi nje na kuingia katika ufalme tukiwa safi. Anatutaka kuwa na kikomo katika utendaji wetu wetu  kibinadamu katika  fahari zetu na hofu zetu.  Ni mwembamba kwa sababu anatutaka tuufunue moyo kwa unyenyekevu na imani kwake, na hasa katika kujitambua wenyewe kwamba, sisi ni wenye dhambi, tunahitaji msamaha wake. Kwa hili, ni mwembamba katika  fahari zetu.  Mlango wa huruma ya Mungu ni mwembamba lakini daima ni  wazi, tena ni wazi kwa kila mtu! Mungu hana upendeleo katika hilo. Daima humkaribisha na kumpokea kila mtu  bila ubaguzi.. Mlango huu ni mwembamba  kwa ajili ya kuzuia fahari yetu na hofu yetu, na hivyo kutuingiza katika  wokovu  unao tiririsha bila kipimo  huruma yake bila kizuizi, na kisha baada ya kupita katika mlango huu, mtu hufunuliwa  mitazamo ya kushangaza ya mwanga na amani.

Papa alieleza na kusema , somo hili la Mlango mwembamba ni mwaliko mwingine unaotolewa na Yesu  kwa watu wote. Mwaliko wa kumwendea , kuvuka vizingiti vya  maisha na kuingia katika furaha kamili .  Na Yesu anamsubiri kila mmoja wetu, bila kujali kama tu wadhambi au la. Anasubiri kutukumbatia katika huruma yake na msamaha  wake.  Ni  Yeye peke yake anayeweza kubadilisha mioyo yetu, Yeye peke yake anaweza kutoa maana kamili ya uwepo wetu, na mwenye kutupa  furaha ya kweli. Baada ya kuingia katika mlango wa Yesu, mlango wa imani na wa Injili, tunaweza kuacha nyuma mitazamo ya kidunia, tabia mbaya, uchoyo na kujitenga ,mbali na wengine . Hutuwezesha kuwasiliana kwa upendo na huruma ya Mungu, na hivyo kuwa na mabadiliko ya kweli katika maisha .  Kuwa na maisha yanayomulikiwa na Mwanga wa Roho Mtakatifu ! Mwanga usioweza kuzimishwa. Papa alisisitiza na kutoa mwaliko kwa wote kuchunguza dhamiri zao iwapo wako tayari kupita katika mlango mwembamba na kuingia dunia  ya furaha ya kweli.

Mwisho alitolea sala kwa Mama Bikira Maria, Mlango wa Mbinguni, akiomba msaada wake ili tuweze kutumia fursa hii ya mwaliko wa Bwana, unaotutaka kuvuka vizingiti vinazozuia kuwa na imani kamili kwa  Yesu na hivyo kuingia katika barabara  ya wokovu, ambayo ni upendo wenye kuokoa, chanzo cha furaha kwa wale ambao, katika upole, uvumilivu na haki, hujitolea sadaka kwa wengine na hasa walio  dhaifu kijamii.








All the contents on this site are copyrighted ©.