2016-08-11 09:08:00

Uwajibikaji wa kimataifa ni kwa mafao ya wengi!


Mafundisho Jamii ya Kanisa; ekolojia na mikakati ya maendeleo endelevu ni kati ya mambo yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati alipokuwa anashiriki katika mkutano wa kimataifa uliokuwa umeandaliwa na Taasisi ya Kanisa Katoliki kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa ijulikanayo kama Bad Honnef, huko Jimbo kuu la Colon, Ujerumani. Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu “Mafundisho Jamii ya Kanisa, ekolojia na maendeleo endelevu”.

Katika tukio hili, Kardinali Oscar Rodriguez Maradiaga alitunukiwa nishani ya heshima katika masuala jamii “Ordo Socialis” kutokana na mchango wake katika mchakato wa kuwashirikisha watu katika sera na mikakati ya maendeleo pamoja na kudumisha utawala bora na mapambano dhidi ya umaskini mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Maradiaga amewahi kuwa ni Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis.

Ajenda za Maendeleo Endelevu kwa mwaka 2030 na changamoto zake kwa Kanisa la Kiulimwengu ni mada iliyofafanuliwa kwa kina na mapana na Kardinali Peter Turkson aliyetumia fursa hii kutoa muhtasari wa mafundisho makuu ya Baba Mtakatifu Francisko katika masuala ya jamii kwa kukazia: utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; umuhimu wa kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini na athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na matumizi sahihi ya sayansi na teknolojia, binadamu na mahitaji yake msingi wakipewa kipaumbele cha kwanza!

Hii inatokana na ukweli kwamba, masuala jamii na utunzaji bora wa mazingira ni mambo yanayogusa pia mchakato wa maendeleo endelevu! Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Sifa iwe kwako, juu ya utunzaji wa mazingira nyumba ya wote, kwa namna ya pekee anakemea ubinafsi, soko huria lisiokuwa na sheria wala kanuni na matokeo yake ni uchu wa mali na faida kubwa kwa hasara ya maskini na wanyonge. Fedha inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu na kamwe isiwageuze watu kuwa ni watumwa wa fedha.

Kardinali Peter Turkson anafafanua kwamba, tangu kulipotokea Mapinduzi ya Viwanda kunako karne ya kumi na nane, idadi ya watu duniani imeongezeka maradufu, lakini hali ya uchumi imeendelea kuzorota siku hadi siku, kiasi cha kuibua changamoto kubwa katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kimazingira. Kutokana na changamoto hizi, Wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kunako mwezi Septemba, 2015 walikutanika Makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani ili kujadili na hatimaye, kupitisha Malengo 17 ya Maendeleo Kimataifa yanayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa ifikapo mwaka 2030.

Mwezi Desemba, 2015 kwa mara nyingine tena, Wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa wakakutana Paris, Ufaransa ili kubainisha sera na mikakati ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Katika mikutano yote hii, Baba Mtakatifu Francisko amewasilisha mawazo na maoni ya Kanisa mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kweli mchakato wa maendeleo endelevu, uweze kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi wa binadamu na maendeleo yake

Lakini Sera na Malengo haya yanaweza kufikiwa ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itajikita katika mshikamano unaoratibiwa na kanuni auni; kwa kupambana na rushwa pamoja na ufisadi, saratani inayokwamisha ustawi na maendeleo ya wengi, hasa maskini na wanyonge ndani ya jamii. Ukweli na uwazi katika matumizi ya rasilimali ya dunia sanjari na mchakato wa kuwahusisha watu wengi katika kuibua, kupanga na kutekeleza sera na mikakati inayohusu maendeleo yao. Soko huria lisimamiwe na kuratibiwa na kanuni maadili, binadamu na mahitaji yake akipewa msukumo wa pekee. Mkazo ni kwa ajili ya: mafao, ustawi na maendeleo ya wengi; mshikamano na maendeleo endelevu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.