2016-08-08 09:55:00

Watawa kujadili siri ya maendeleo Barani Afrika!


Watawa wa mashirika ya kitume na kazi za kimissionari kutoka katika nchi kumi za Kiafrika,  tarehe 17- 18 Oktoba, 2016 watakusanyika Jijini Nairobi, Kenya ili kujadili siri ya maendeleo endelevu Barani Afrika. Mkutano huu umeandaliwa na Mfuko wa Conrad N. Hilton. Mkutano huu unaotarajiwa kuhudhuriwa na watawa 160 utaongozwa na kauli mbiu “ Siri ya maendeleo endelevu Barani Afrika”. Mkutano huu utatanguliwa na Ibada ya Misa Takatifu itakaoongozwa na Askofu mkuu Charles Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya na Sudan ya Kusini.

Sr. Rosemarie Nassif, Mkurugenzi wa Programu wa Mfuko wa Conrad N. Hilton anasema, lengo lao kuu ni kushirikiana na wadau mbali mbali ili kuweza kuibua mpango kazi wa pamoja kwa ajili ya mchakato wa maendeleo endelevu Barani Afrika. Kutokana na mwelekeo huu, Mfuko wa Conrad umewaalika wadau mbali mbali kutoka katika taasisi za fedha na mashirika yasiyo ya kiserikali kushiriki katika mkutano huu.

Watawa katika maadhimisho ya Mkutano huu wa siku mbili watapata nafasi ya kushirikisha fursa na changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo katika mchakato wa maendeleo endelevu Barani Afrika.  Mwishoni, wataweka mpango mkakati utakaotekelezwa ili Bara la Afrika liweze kucharuka kwa maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.