2016-08-08 09:10:00

Papa aonya : Sanda haina mifuko!


Baba Mtakatifu Francisko akiwahutubia mahujaji na wageni katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 7 Agosti 2016, alionya dhidi ya tabia ya kushikamana  na mali na  fedha akisema , wakati wa kifo yote hubaki hapa dunia, haijalishi kama una mali nyingi au  fedha , maana sanda halina mifuko ya kubeba mali. Papa aliasa wakati akitafakari  kifungu cha Injili  ya Luka  12.32-48, ambamo Yesu  aliwazungumzia wanafunzi wake juu ya  itakavyokuwa siku ya mwisho ya kukutana nae. Kukutana kunakopaswa kuwa kichochea na msukumo kwa mtu kuishi kwa wema. Yesu aliwahimiza wanafunzi wake kusaidia wengine na kujiwekea akiba  katika mfuko usiochakaa, yaani kujiwekea hazina salama mbinguni  ambako hakuna Mwizi wala nondo wa kuitafuta.

Papa alisisitiza kwamba huu ni mwaliko wa thamani wa majitoleo ya sadaka katika kazi za matendo ya huruma  na  sio kuweka tumaini katika mambo ya kidunia yanayopita kwa kasi kama upepo . Ni mwaliko wa kujinasua na ubinafsi, na kuishi kwa mujibu wa mantiki ya Mungu,  kutoa kipaumbele  kwa wengine, ni mantiki upendo. Na inawezekana kuishi hivyo bila kushikamana na  fedha, maana hata kama tungekuwa na mali nyingi  na fedha  nyingi, saa ya mwisho ya maisha ikifika,  hatuwezi kuvichukuahuko tuendako baada ya maisha ya kidunia.  Papa alieleza na kukumbusha kwamba,  "sanda hana mifuko."

Kwa hiyo akasema , mifano mifupi mitatu iliyotolewa na Yesu katika fungu hili la Injili:  kuweka akiba mbinguni; Watumishi waangalifu ; na mtumishi aminifu na asiye aminifu ,  ni somo juu ya usimamizi wa mali, ambamo tunaonywa  kwamba , ni muhimu: kuangalia na kuwa macho na aminifu katika maisha.  Alinukuu"Heri  watumishi wale ambao Bwana wao atakaporudi atawakuwa wako tayari”. Papa alitafakari aya hizo akisema , zinaonyesha  furaha ya kusubiri katika imani Bwana ,  katika mtazamo wa huduma, na hasa huduma kwa maskini. Papa alieleza na kuomba msaada wa Ulinzi wa kimama wa  Bikira Maria.

Na baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Papa  akisalimia makundi mbalimbali, aliutumia muda huo kutoa ombi lake kwa mara nyingine  kwa ajili ya wahanga wa machafuko ya Kisiasa nchini Syria akiomba amani . Alionyesha kujali kwamba, taarifa mbaya zinaendelea kusikika tokea Syria jinsi raia wanvyoathirika na vita na hasa katika eneo la  Aleppo. Alikemea dhuluma hizo  akisema kuwa  haikubaliki kwamba watu wanyonge wakiwemo  watoto wengi wanafanywa kuwa sadaka ya machafuko yanayofanywa na watu wenye roho ngumu . Kafara hao wanatamani amani itawale miongoni mwao lakini wananyiwa haki hiyo na kundi dogo la watu wenye mabavu.  Kwa maneno hayo alitoa mwaliko kwa watu wote.kupitia sala kushikamana na raia wema wa Syria, wake kwa waume  , na aliyakabidhi yote chini ya Ulinzi wa Kimama wawa Mama Maria.  Aliwasihi wote kukaa kimya kwa muda mfupi  na kisha wakasali sala ya Salaam Maria. 








All the contents on this site are copyrighted ©.