2016-08-07 11:05:00

Ijumaa ya huruma ya Mungu nchini Poland


Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Poland wakati wa maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani, ilipambwa kwa namna ya pekee na ukimya, sala, tafakari pamoja na matendo ya huruma kwa kutembelea hospitali ya watoto Jimbo kuu la Cracovia, yaliyomwilishwa Ijumaa ya tarehe 29 Julai 2016, Ijumaa ambayo imeguswa na kushuhudiwa na huruma ya Mungu! Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amejiwekea utaratibu wa kutekeleza tendo la huruma walau kila Ijumaa anapopata nafasi!

Ni ushuhuda unaotolewa na Askofu mkuu Salvatore Rhino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji Mpya katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano kuhusu hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Poland kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa vijana wa kizazi kipya! Siku hiyo ya Ijumaa, Baba Mtakatifu alitembelea kambi za mateso na mauaji ya kikatiliki huko Auschwitz- Birkenau; akatembelea Hospitali ya Watoto na kusalimiana na watoto wagonjwa na hatimaye, jioni akashiriki kikamilifu na vijana katika maadhimisho ya Njia ya Msalaba, ambayo kwa Siku ya Vijana Duniani huko Poland, yalijikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, sehemu muhimu sana ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Askofu mkuu Rino Fisichella anakumbusha kwamba kusali kwa ajili ya kuwaombea wafu ni sehemu ya matendo ya huruma: kiroho na hili limetekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alikaa katika hali ya ukimya na kusali kwa ajili ya watu walioteswa na kuuwawa kikatili kwenye kambi hizo! Hapa ni mahali ambapo utu na heshima ya binadamu vilitelekezwa, changamoto na mwaliko kwa walimwengu wa sasa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka huu huko Poland, limekuwa ni tukio la neema katika mchakato wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Vijana wamefanikiwa kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa njia ya sala, tafakari, katekesi, ibada na maadhimisho ya Mafumbo mbali mbali ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko pamoja na vijana wamepata nafasi ya kupitia katika Lango la huruma ya Mungu, baada ya kufanya maandalizi yote yanayohitajika ili mwamini aweze kupata rehema kamili!

Askofu mkuu Fisichella anasema, kulikuwepo na Maaskofu 800 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, na kati yao walihusika na kutoa katekesi za kina kwa vijana kwa kuwataka vijana kuwa kweli ni vyombo, mashuhuda na mitume wa huruma na upendo wa Mungu kwa walimwengu. Itakumbukwa kwamba, maadhimisho haya yalikuwa yanaongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. Katekesi zilipania kugusa undani wa maisha ya vijana, ili kweli waweze kufundwa kadiri ya huruma na upendo wa Mungu, tayari kushuhudia tunu hizi msingi katika maisha yao ya kila siku. Vijana wanahamasishwa kutekeleza ndani mwao changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Poland, ili kuleta mageuzi yanayokusudiwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wa vijana. Vijana wawe kwelini moto wa kuotoea mbali na kamwe wasikubali kupokwa matumaini haya na wajanja wachache anasema Askofu mkuu Rino Fisichella.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 yatafanyika nchini Panama. Ikumbukwe kwamba, Bara la Afrika na Amerika ya Kusini ni maeneo ambayo yana idadi kubwa sana ya vijana. Ni maeneo ambayo imani bado ina nguvu katika maisha ya watu, hata kama kuna changamoto na magumu wanayowasibu vijana katika maeneo haya, kumbe Kanisa linapaswa kuwa makini na macho ili kuzitambua changamoto hizi na kuzifanyia kazi mara moja.

Panama ni taifa changa, lakini thabiti katika imani, kumbe linaweza kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa ujenzi wa maisha bora kwa raia wake. Baba Mtakatifu anawataka vijana kutoka Amerika ya Kusini waweze kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa la Kristo na wala si watu wa kuja au kupita tu! Panama, kijiografia imekaa mahali pazuri zaidi pa kuweza kuwaunganisha vijana kutoka Amerika ya Kaskazini na Amerika ya Kusini, ili kujenga Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.