2016-08-06 09:50:00

Kumbu kumbu ya Miaka 71 ya shambulio la Atomic Japan!


Kuanzia tarehe 6 – 9 Agosti 2016, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 71 tangu miji ya Hiroshima na Nagasaki iliyoko nchini Japan, iliposhambuliwa kwa mabomu ya  Atomic na kusababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Kunako mwaka 1996 lilipitisha azimio la kuacha utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia kwani zina madhara makubwa kwa binadamu. Hii bado ni changamoto kubwa kwa binadamu katika ulimwengu mamboleo!

Maadhimisho haya yanapewa uzito wa pekee na viongozi wa kidini, wanasiasa na wapenda amani nchini Japan kwa kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika tafakari na makongamano mbali mbali ili kubaini madhara ya vita na umuhimu wa kujenga na kudumisha majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi ili kulinda: haki msingi za binadamu, maisha, utu, ustawi na maendeleo ya wengi.

Padre Michael Czerny, afisa kutoka Baraza la Kipapa la haki na amani amekuwepo nchini Japan kushiriki katika maadhimisho haya  kama shuhuda wa mshikamano na matumaini. Kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 6 Agosti 2016, Kanisa linapoadhimisha pia Sherehe ya kung’ara kwa Bwana, changamoto na mwaliko kwa waamini kusikiliza kwa makini sauti ya Kristo na kumfuasa, tayari kuambata na kutekeleza mapenzi ya Mungu ambaye ni huruma na upendo katika maisha ya mwanadamu kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Padre Michael Czerny katika ujumbe alioutoa kwa niaba ya Baraza la Kipapa la haki na amani anasema, tarehe 8 Agosti 2016 Kanisa pia linafanya kumbu kumbu ya miaka 38 tangu alipofariki dunia Mwenyeheri Paulo VI. Wakati alipolihutubia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1965 aliitaka Jumuiya ya Kimataifa kukomesha vita duniani, lakini hata leo hii kuna watu wanaoendelea kuteseka, kufariki na kunyanyasika kutokana na vita.

Siku hii imekuwa maalum kwa ajili ya kuwambuka na kuwaombea waathirika wa mashambulizi ya mabomu ya Atomic huko Hiroshima na Nagasaki bila kuwasahau watu wanaoendelea kupoteza maisha kutokana na vita, mashambulizi ya kigaidi na mipasuko ya kijamii, hasa wakati huu Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 71 tangu Miji ya Hiroshima na Nagasaki iliposhambuliwa kwa mabomu ya Atomic.

Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuacha dhambi na ubaya wake, ili kutoa fursa kwa: neema, huruma na upendo wa Mungu kusamehe na kuponya madonda ya vita, chuki na uhasama. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kushangazwa na Mwenyezi Mungu kwa kuafungulia watu malango ya huruma na upendo wake, ili kuwashirikisha watu maisha yake ya Kimungu.

Kanisa kwa namna ya pekee, linaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu kama kiini cha ufunuo wa Yesu Kristo. Waamini wamesali kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kufuta dhambi zao kwa kuwamiminia mto wa rehema na huruma, ili watu waweze kuzama humo! Kumbu kumbu ya miaka 71 ya mashambulizi ya Mabomu ya Atomic sanjari na Sherehe ya kung’ara Bwana na Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu iwe ni fundisho na mwongozo wa maisha ili kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.