2016-08-06 14:48:00

Hali ya kisiasa na kiuchumi Zimbabwe ni tete!


Viongozi wa Makanisa nchini Zimbabwe katika tamko lao la pamoja wanasikitishwa sana na hali ngumu ambayo wananchi wanakabiliana nayo: kiuchumi, kisiasa na kijamii kiasi ambacho kinaanza kusababisha machafuko ya kisiasa na kijamii sehemu mbali mbali nchini Zimbabwe. Katika miaka ya hivi karibuni viongozi wa Serikali na kisiasa nchini Zimbabwe wameshindwa kusikiliza na kujibu kilio na kero za wananchi wao.

Kumekuwepo na uvunjaji mkubwa wa Katiba ya nchi; rushwa, ufisadi na ubaguzi pamoja na mipasuko ya kisiasa hata ndani ya vyama vyenyewe, mambo ambayo pia yana athari kubwa katika umoja na mshikamano wa kitaifa! Viongozi wa Makanisa nchini Zimbabwe wakiwa wanasukumwa kwa namna ya pekee na dhamana waliyokabidhwa na Kristo Yesu, wanahamasishwa kusimama kidete ili kulinda, kutetea na kudumisha mafao ya wengi pamoja na kukemea ukosefu wa haki msingi za binadamu.

Viongozi wa Makanisa wanaitaka Serikali ya Zimbabwe kusikiliza na kujibu kilio cha wananchi wake kwa kutenda kwa haki na huruma kwa ajili ya maskini na wananchi wengi wa Zimbabwe wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na umaskini wa hali na kipato! Viongozi wa Makanisa wanapinga kwa nguvu zote matumizi makubwa ya nguvu kutoka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama dhidi ya wananchi.

Viongozi wanaitaka Serikali kuhakikisha kwamba, vyombo hivi vinawalinda raia na mali zao badala ya kuwa ni vyombo vya kunyanyasa na kuwatesa watu wasiokuwa na hatia. Wananchi nao wahamasishwa kuzingatia utawala wa sharia, amani na utulivu wanapodai haki zao. Serikali haina budi kulivalia njuga suala la ukosefu wa fursa za ajira nchini Zimbabwe ambao kwa sasa umefikia kiasi cha asilimia 80%. Serikali inapaswa kuwajibika ili kuwajulisha wananchi kashfa ya upotevu wa kiasi cha dolla za Kimarekani billioni 15 pamoja na kashfa ya Serikali kushindwa kuwalipa ujira wafanyakazi wake.

Mashirika na Makampuni ya Umma yanaendelea kuporomoka na kufilisika kutokana na rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma unaofanywa na baadhi ya viongozi waliopewa dhamana na madaraka ya kusimamia na kuongoza Mashirika na Makampuni haya. Serikali imeshindwa kuwashirikisha wadau mbali mbali katika sera na mipango yake na matokeo yake ni uwepo wa changamoto za kikatiba zinazoendelea kutolewa na wananchi. Kuporomoka kwa biashara ya ndani na nje kunaendelea kugumisha maisha ya wananchi wengi wa Zimbabwe. Vizuizi vya barabarai vinaendeleza rushwa.

Kutokana na changamoto zote hizi, wananchi wengi wa Zimbabwe wamekosa Imani na Serikali yao. Viongozi wa Makanisa wanaitaka Serikali kuanzisha mchakato wa majadiliano na wadau mbali mbali kwa ajili ya ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa na hivyo kuondokana na mwelekeo wa sasa unaotaka kuwanyanyasa viongozi wa kidini. Vitendo vya namna hii vinaweza kutafsiriwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kutaka kuwafunga mdomo viongozi wa Makanisa. Hapa kuna hatari kubwa inayoweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Serikali kwa upande wake itekeleze dhamana na majukumu yake vyema kwa wananchi. Waamini wa Makanisa mbali mbali ambao ni chumvi na mwanga wa taifa kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea umoja na mshikamano wa kitaifa; haki, amani na utulivu.

Viongozi wa kidini kutoka Zimbabwe wanakaza kusema, wanataka Serikali inayojikita katika utawala wa sharia unaozingatia Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni Sheria mama. Wananchi wa Zimbabwe wawe na hofu ya Mungu kwa kujikita katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, daima wakitekeleza ile kanuni ya dhahabu kujipenda na kuwapenda jirani zao. Mwishoni, viongozi wa Makanisa wanawaombea wananchi wote wa Zimbabwe waweze kuwa na ujasiri, imani, matumaini na mapendo, ili kuweza kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zilizoko mbele yao kwa sasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CANAA.








All the contents on this site are copyrighted ©.