2016-08-06 16:14:00

Hakuna hekima mbadala!


Mtakatifu Augustino wa Hippo anasema ‘imani hufungua mlango wa ufahamu na kukosa imani huufunga’ Ndugu zangu, somo la kwanza latoka kitabu cha Hekima ya Solomoni, katika sehemu ya tatu ya kitabu hiki. Hapa kazi ya Mungu inatukuzwa katika historia ya taifa teule, ikiangalia hasa uhuru wao toka utumwani Misri. Dhumuni na lengo la kitabu hiki ni kuwatahadharisha Wayahudi wenye elimu ya Mungu na hatari ya elimu dunia. Angalizo hili limetokea baada ya kujichanganya na watu na vitu vilivyo mbali na Mungu. Mwandishi anaandika ili kuwakinga na upotevu. Hekima ya kweli ni Mungu, kupitia njia ya sala. Hakuna hekima mbadala.

Kwa ufupi, katika kitabu hiki twapata habari juu ya sadaka ya Pasaka, juu ya habari ya kutoka utumwani – Kut. 12 – kama sadaka ya kwanza ya ukombozi wa mwanadamu. Ni sikukuu ya kukumbuka fadhila ya ukombozi. Somo la pili linatoa fundisho kwa ajili ya wakristo wapya ili kuwatahadharisha juu ya imani yao mpya, mfano kutambua wazi tofauti kati ya sadaka ya wanyama na sadaka ya Kristo, tofauti kati ya ukuhani wa Kristo anayeondoa dhambi za watu n.k na viongozi wa kawaida katika taifa la Israeli. Somo la injili latoka injili ya Luka na kwa ujumla injili yaongea juu ya wakristo wasio Wayahudi na tunaona habari juu ya huruma ya Yesu – aliwahurumia wakosefu. Lk. 15:1-2, anasamehe dhambi - Lk 15:11-32, mpole 1:51-53. Ni Injili iliyojaa shukrani kwa Mungu kwa mambo yote aliyofanya kwa ajili ya kuwakomboa watu na yaonesha furaha kubwa ya kiroho juu ya matendo ya wokovu - Lk. 2:14, 5:26.

Katika somo hili tunasikia uzuri wa neno la Mungu unaojengwa kwenye matumiani na mwanzo wa somo tunasikia msiogope enyi kundi dogo. Halafu Yesu anaongea juu ya hatari ya mali na haja ya uaminifu na mwaliko wa kujiweka tayari kwa wa ujio wa Bwana. Mwito wa Kikristo uko wazi hapa – tunao Ufalme wa Mungu – msiogope.

Kwa kifupi, ufahamu unatuwajibisha. Angalia masomo yetu yote ya leo na ujumbe uliopo unajirudia. Na ndiyo sababu baada ya kutufundisha, atukumbusha kuwa tayari na viuno viwe vimefungwa. Amani ya ufalme na uwajibikaji ni sifa zinazowekwa bayana na Yesu. Ndiyo maana Yesu anasema msiogope. Wito wa Yesu ni kutoa jibu na kuwajibika. Uelewa huo kama ulivyo katika somo la kwanza watafsiri maana ya sadaka ya ukombozi. Hivyo katika somo la pili twaona jibu hilo, jibu la imani/mababu zetu katika Agano la Kale – angalia imani ya Abrahamu na Sara – aliamini na kuwa tayari kuondoka alipokuwa tayari kutoa sadaka ya mtoto wake wa pekee. Hata Mt. Paulo mwalimu wa mataifa anashangaa imani ya namna hiyo – Rom. 4:18. Sasa uelewa wa maisha ya imani utusaidie kuelewa kwanini Yesu asema msiwe na woga.

Tulipoadhimisha Mwaka wa Imani tulichagizwa na mwaliko wa wongofu wa kweli, uliofanywa upya na Bwana, Mwokozi pekee wa ulimwengu. Katika Fumbo la kifo na ufufuko wake, Mungu amefunua katika ukamilifu wake upendo unaookoa na kutualika sisi kwa uongofu wa maisha kwa njia ya maondoleo ya dhambi – Mdo. 5:31. Kwa mtakatifu Paulo, upendo huu unatupeleka kwenye maisha mapya ‘basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima – Rum. 6:4’.

Kwa njia ya imani maisha haya mapya yanaunda uhai wote wa mwanadamu kadiri ya uhalisia mpya usiotetereka wa ufufuko. Kwa kadiri ile ambayo, kwa uradhi wote mtu anashiriki fumbo hili, mawazo ya mwanadamu na shauku zake, mtazamo na tabia zake zinaanza kutakaswa na kubadilisha taratibu katika safari ambayo kamwe haikamiliki katika maisha haya. Imani itendayo kazi kwa upendo –Gal. 5:6 inakuwa ni kigezo kipya cha uelewa na utendaji unaoyabadilisha maisha yote ya mwanadamu – Kol. 3:9-10, Efe. 4:20, 2Kor. 5:17. Hakika leo tunaalikwa kuitambua hekima hii Mungu, kutumia muda wetu kutambua imani hiyo vizuri na matendo ya imani na namna ya kuwekeza hazina yetu. Tukifanya hivyo tutaenzi neno la Mungu jumapili hii ya leo. Na hekima ya Mungu ni kumtambua yeye na mpango wake wa ukombozi kama ulivyotufikia kwa njia ya Mwanawe.

Tumsifu Yesu Kristo.

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.