2016-08-06 15:03:00

Fanyeni mageuzi haraka ili uchaguzi uwe huru na wa haki!


Viongozi wa kidini nchini Kenya wanaounda Jukwaa la Mageuzi ya Uchaguzi nchini Kenya hivi karibuni katika mkutano wake, limeitaka Serikali pamoja na wadau mbali mbali kujenga utamaduni wa majadiliano ili kuimarisha mchakato wa mageuzi ya sheria za uchaguzi mkuu, kuwawajibisha wabunge pamoja na kuhakikisha kwamba, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa vinadumishwa kabla, wakati na baada a uchaguzi mkuu nchini Kenya unaotarajiwa kufanyika kunako mwaka 2017.

Jukwaa la Mageuzi ya Uchaguzi mkuu nchini Kenya linavitaka vyombo vinavyohusika kuhakikisha kwamba vinashirikiana kwa karibu zaidi ili kupata suluhu ya matatizo na changamoto kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Kenya, ili uweze kuwa huru na wa haki. Busara na masilahi ya taifa yapewe kipaumbele cha kwanza kwa kujikita katika majadiliano yatakosimamiwa na viongozi wakuu wa Bunge, ili kuwawezesha wananchi kujiandaa kwa uchaguzi mkuu hapo mwakani.

Jukwaa la Mageuzi ya Uchaguzi mkuu nchini Kenya linaipongeza Tume kwa kuanza kukusanya maoni ya wananchi, lakini inapaswa kutekeleza dhamana hii kwa haraka zaidi ili kuondokana na njama au ujanja wowote unaoweza kutumiwa na wanasiasa kuvuruga uchaguzi mkuu. Jukwaa hili litaendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali ili kuhakikisha kwamba, Tume hii inatekeleza wajibu wake barabara. Mabadiliko yafanywe, ili hatimaye Tume mpya iweze kuundwa na wala kusiwepo na wanasiasa wanaotaka kubadili tarehe ya Uchaguzi mkuu kwa mwaka 2017.

Jukwaa la Mageuzi linakaza kusema, hapa kuna haja ya kuimarisha taasisi itakayoundwa, ili kuboresha mfumo mzima wa uchaguzi mkuu, ili matokeo yaweze kukubaliwa na wengi zaidi. Ikiwezekana Tume hii iwe imeundwa rasmi ifikapo mwezi Januari 2017, tayari kufanya maandalizi muhimu kwa ajili ya uchaguzi mkuu.

Jukwaa la Mageuzi ya Uchaguzi mkuu nchini Kenya linasema, litasimama kidete kuendeleza mchakato wa uragibishaji, uwajibikaji, ukweli na uwazi na kutaka liwepo Daftari la Wapiga kura kwa wakati muafaka. Litaendelea kuwajengea wadau mbali mbali uwezo wa ndani wa kufanya tafiti, kuhifadhi nyaraka pamoja na kuendelea kujifunza uratibu na teknolojia ya uchaguzi.

Viongozi hawa wa kidini watatumia taasisi zao kutoa elimu ya urai, kuhimiza haki na amani pamoja na kuwahamasisha raia kutekeleza vyema wajibu wao wa kiraia kwa kushiriki mchakato mzima wa upigaji kura. Wataendeleza majadiliano na makongamano katika ngazi mbali mbali, ili kupima misingi ya ukweli na uwazo miongoni mwa wanasiasa. Ni vyema ikiwa kama viongozi wa Serikali watataja mali yao na wafanyakazi wa majimbo kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao. Mwishoni wanakaza kusema, wataendelea kuhimiza na kusimamamia utekelezaji wa sheria za uchaguzi mkuu nchini Kenya.

Mwishoni, viongozi wa kidini wanawataka wananchi wote wa Kenya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi mkuu, kwa kusali pamoja na kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu na maridhiano kati ya watu.

Na Padre Richard  A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.