2016-08-06 14:36:00

Chuki na uhasama vinahatarisha amani na mafungamano ya kijamii


Monsinyo Janusz Urbanczyk, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Vienna anasema inasikitisha kuona kwamba, kuna mwelekeo wa chuki na uhasama dhidi ya wananchi wanaotoka katika nchi ndogo hali ambayo inaweza kuhatarisha amani, utulivu na mafungamano ya kijamii. Monsinyo Urbanczyk ameyasema hayo hivi karibuni wakati akichangia mada kuhusu taarifa ya hali ya watu wachache Barani Ulaya kwenye mkutano wa Shiirkisho la Usalama na Maendeleo Barani Ulaya, OSCE.

Monsinyo Urbanczyk anakaza kusema, lugha ya chuki, matusi na uhasama inaendelea kusikika sana miongoni mwa wananchi wa Ulaya hali ambayo kama haitaweza kudhibitiwa kikamilifu na haraka iwezekanavyo inaweza kusababisha kinzani, mipasuko na hata maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano ili kuwawezesha watu kuishi katika utulivu kwa kuheshimiana na kuthaminiana licha ya tofauti zao za mahali anapotoka mtu, dini au imani yake.

Nchi wanachama wa OSCE zinapaswa kuepuka sera za ukandamizaji na ubaguzi wa watu kutokana na sababu mbali mbali; mambo ambayo wakati mwingine yanakumbatiwa na sheria za nchi. Haya ni hatari sana kwani yanaweza kuchochea hali ya watu kukosa maridhianano na uelewano na matokeo yake maafa makubwa. Vitendo vya baadhi ya wanasiasa kutumia maneno ya chuki na uhasama dhidi ya wahamiaji na wageni wanaoishi Barani Ulaya kama njia ya kujijenga kisiasa ni hatari sana kwa mafungamano ya kijamii kama ambavyo inajionesha kwa baadhi ya nchi.

Tabia hii idhibitiwe na badala yake wananchi wahamasishwe kujikita katika mchakato unaopania kudumisha haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo yake: kiroho na  kimwili. Vijana wa kizazi kipya wafundwe na kupewa elimu makini inayojikita katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano baina ya watu, ili kuimarisha uelewano kati ya watu.

Ni wajibu wa familia na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanasiaidia kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kijamii na kitamaduni miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Watu wajenge mwamko wa kuheshimu haki msingi za binadamu kwa kukuza umoja na mshikamano pamoja na kuheshimu tofauti za kidini na kiimani; mambo ambayo ikiwa kama hayaheshimiwa na wote, yanaweza kuwa ni chanzo cha misigano na chuki za kidini; matokeo yake ni vita, nyanyaso na dhuluma za kidini bila kusahau vitendo vya kulipizana kisasi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.